NA ABOUD MAHMOUD
WAJUMBE wa mkutano mkuu wa Chama cha Wasanii wa Muziki wa Kizazi Kipya Zanzibar (ZFU), wamemchagua tena Mohammed Abdullah ‘Laki’ kuwa rais wao kwa kupata kura 34.
Uchaguzi huo ulifanyika kwenye ukumbi wa Studio za Serikali Rahaleo mjini Unguja, Laki ataiongoza nafasi hiyo kwa kipindi cha pili kwa miaka mitatu.
Katika kinyang’anyiro hicho Laki aliwashinda wagombea wenzanke akiwemo Kassim Omar ‘Mashmale’ aliyepata kura 8 na Felista Phili alipata kura 1,ambapo katika kura 44 kura moja iliharibika.
Wengine waliochaguliwa ni Faiza Iddi Ferouz kuwa Makamu wa rais kwa kupata kura 25 huku kura 17 zilienda kwa wapinzani wake ambapo kati ya kura 44 mbili zimeharibika.
Wengine ni Salum Zarafi Said katibu mkuu wa chama hicho na Suleiman Juma Suleiman amekua katibu msaidizi.
Mara baada ya kuchaguliwa kushika nafasi ya urais,Laki alisema atashirikiana na wasanii wenzake katika kufikia malengo waliyoyakusudia ikiwemo kukuza fani yao hiyo.
Laki aliwashukuru wajumbe waliomchagua na kusema kwamba kuchaguliwa kwake kunatokana na utendaji wake aliokuwa nao pamoja na mashirikiano anayoyatoa kwa wasanii hao.