LIGI Kuu ya Zanzibar imerejea tena viwanjani baada ya kusimama kwa wiki kadhaa kufuatia kuwepo kwa michuano ya Kombe la Mapinduzi ambayo ilifikia tamati Januari 13 mwaka huu.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Bodi ya Ligi, michuano hiyo itakuwa ikiendelea Unguja na Pemba ikiwa imeanzia na mzunguko wa tisa.
Tunachukuwa nafasi hii kuzitakia kila la heri klabu zote 12 za ligi hiyo ili ziendelea na ngarambe hizo ambazo ndizo zinazotoa mwakilishi wa Zanzibar kwenye michuano mikubwa ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Kubwa tunalowaambia wenzetu wa Bodi ya Ligi kuwa makini zaidi inapopanga ratiba ya mechi hizo kuhakikisha inakwenda vizuri ili kumalizika kwa wakati kwa kadri inavyowezekana.
Watendaji wa Bodi ya Ligi wanatakiwa kuumiza vichwa ili kupanga ratiba nzuri, ambayo huko mbele haitakuwa na maswali mengi na majibu machache kutoka kwa wadau wa soka, ambao mara kwa mara wamekuwa wakiitupia lawama bodi hiyo.
Mbali na hilo, tungelipenda kuzikumbusha timu zinazoshiriki ligi kuendelea na kasi ya ushindani na msisimko ili kuendelea kuwavutia mashabiki ambao bado wana kumbukumbu ya ushindani uliokuwepo kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi.
Sote ni mashahidi kwa namna michuano ya Kombe la Mapinduzi ilivyokuwa na ushindani na kukonga nyoyo za mashabiki waliokuwa wakiishuhudia michuano hiyo.
Tumeona na kushuhudia soka ya nguvu na viwango kutoka timu zote tisa zilizokuwa zikishiriki michuano hiyo na hilo ndilo lililokuwa chachu ya kuwepo kwa mashabiki wengi uwanjani kwa takribani ya kila mchezo.
Sasa ni matarajio ya wapenzi wengi wa soka kuona ligi yetu nayo inakuwa bora kuanzia kwa timu kuwa bora, waamuzi kutochezesha kwa upendeleo au ubabaishaji na Bodi ya Ligi kuhakikisha ratiba na mambo mengine yanakwenda vizuri ili kumpata bingwa halali.
Msimu uliopita waamuzi walikuwa tatizo kidogo na kulikuwepo na malalamiko kadhaa yalioelekezwa kwao, hivyo Bodi ya Ligi ambao ndio wasimamizi wakuu wa ligi hiyo, wanatakiwa kuwa makini katika kuwapanga na kikubwa wanatakiwa kuendelea kutoa mafunzo kwa waamuzi hao.
Ligi ikiwa na ushindani wa kweli sio ule wa baadhi ya timu kubebwa, utasaidia kuongeza mashabiki viwanjani, kwani huwa hawana nafasi ya kwenda na matokeo yao na badala yake wanayakuta huko huko.
Ushindani wa ligi pia utasaidia kuvutia wadhamini ambao wanahitajika katika maendeleo ya soka na michezo kwa ujumla.