AUSI A. ALI, (Mtafiti mambo ya bahari)

VITO vya lulu na marijani ni madini ambayo Mwenyezi Mungu (S.W), ameyataja katika kitabu cha kur-an katika suratul Rahman katika aya ya 22 kutokana na umuhimu wake wa matumizi katika fani ya mapambo mbali mbali ambayo hutumiwa na wanaadamu.

Hata hivyo, ukweli ni kwamba wanaadamu wanafahamu mambo machache tu katika matumizi ya madini ya lulu na marijani, ambayo Mwenyezi Mungu ameyataja katika kitabu chake hicho.

Nichukue fursa hii kumpongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi ambaye ameingia na sera ya uchumi wa buluu, na kwa umuhimu wake ameunda wizara maalum.

Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi haikuwepo kabla na kwa kweli wizara hiyo ilishangaza watu wengi baada ya kuundwa kwake na kutangazwa kwake.

Ilishangaza watu siyo kwamba ni kioja hapana, bali ilishangaza watu kwa kuona jina jipya la wizara na malengo yake ambayo yamekusudiwa ambayo yanayoingia akilini.  

Tukiliangalia jina la wizara tunaona limekusanya maneno matatu makuu nayo ni uchumi buluu na uvuvi. Uchumi maana yake ni uzalishaji mali, buluu maana yake ni rangi maalumu iliyopwaya kutoka weusi uliyokoza na kwa hapa ni rangi ya kina kirefu cha maji ya bahari.

Uvuvi maana yake ni mbinu nyingi za kiufundi ambazo hutumiwa na wavuvi kwa lengo la kumfanya kiumbe wa baharini kama vile samaki ahadalike na kuingia katika mtego.

Bila shaka kwa hapa unakusudiwa uvuvi wa kisasa na wa kina kirefu cha maji ya bahari. Kwa kweli Zanzibar imebarikiwa kuwa na eneo kubwa la bahari hasa upande wa kusini mashariki ya bahari ya hindi.

Wataalamu wa mambo ya uvuvi wanaeleza kwamba bahari ya Zanzibar ina samaki wengi sana tena waajabu, yaani tokea kuumbwa kwa dunia samaki hao hawaja vuliwa ipasavyo kwa kutumia utaratibu unaofaa.

Bila shaka raslimali hii ikiwa itatumika vizuri basi inaweza kusaidia sana kuleta maendeleo ya kiuchumi kwa wavuvi na taifa kwa ujumla.

Tukiangalia bahari ya Zanzibar tutaona kuwa ina mambo mengi yanayohusiana na mali. Mali hizo ni kama vile samaki ‘sea horse’, majongoo, makombe na mwani.

Ukitoa ‘sea horse’ mali hizo karne nyingi zilizopita zikitumka kama chanzo kikuu cha uchumi cha kuendeshea maisha.

Zanzibar miaka mingi iliyopita kabla ya kuja sekta ya utalii katika miaka ya hivi karibuni ilitegemea sana rasilimali za karafuu pili pili hoho, makombe majongoo na mwani hizo ndizo zilikuwa rasilimali za msingi kwa Zanzibar ambazo zikisafirishwa n’gambo kwa ajili ya kupata fedha za kigeni.

Lakini kwa hivi sasa hali imebadilika kwani inasemekana kwamba utalii ndiyo sekta ya kwanza ambayo huchangia kiasi kikubwa cha fedha za kigeni.

Kufuatia kubuniwa kwa wizara mpya ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi hivi, kumekuwa na hamasa kubwa ya matarajio kwamba nchi yetu itakuwa na kichocheo kipya cha kukuza uchumi.

Bahari kama lilivyo jina lake, kwa hakika imekusanya mambo mengi ndani yake, yapo mambo ambayo tumezoea kuyaona na kuyafahamu matumizi yake, lakini pia yapo mambo ambayo tumezoea kuyaona lakini hatuyafahamu matumizi yake.

Hata hivyo, hali kama hiyo ni ya kawaida katika maisha ya mwanadamu ndiyo maana kuna vyuo vingi vya kujifunzia watu. Ninasema haya nikiwa na maana maalumu kama nitakavyo onesha.

Kwa hakika nadharia iliyobuniwa ya uvuvi wa bahari kuu itakuwa na faida kubwa sana nchini, iwapo mipango inayobuniwa itakamilika na kutekelezwa kwa ufanisi.

Tukiacha kuzungumzia uvuvi wa bahari kuu na kuanza kutazama uvuvi wa kawaida ambao tumeuzoea na kuurithi kutoka kwa mababu zetu kavile uvuvi wa majongoo (sea cucumber).

Uvuvi huu nao unafaida kubwa sana katika kuchangia pato la taifa kwa jumla na pia ni ajira kubwa ya asili kwa watu wanaojishughulisha na kazi hiyo.

Hata hivyo, kazi hiyo inaweza kuwa bora zaidi na kubadili hali za wa wavuvi kimaisha na pia kuchangia pato la taifa iwapo itafanywa kitaalamu kwa kupewa elimu ya kisasa watu ambao wanafanya kazi hiyo na kuacha kuifanya kwa mazoea kama ilivyo hivi sasa.

Tukiangalia zao la mwani (sea weed) tutaona kuwa kwa sehemu kubwa utendaji wake unaridhisha, hata hivyo juhudi za ziada zinahitajika kwani inaonekana kuwa juhudi za wakulima wa zao hilo inapunguwa.

Ukulima wa mwani ulishika kasi kubwa visiwani mnamo miaka ya 1989-1999 na kuzalishwa matani kwa matani na kusafirishwa nje ya nchi, lakini kwa hivi sasa hali inatia wasi wasi sijui kwa sabubu gani.

Makombe ‘sea shells’ ni biashara ya asili ambayo imekuwepo tangu enzi na enzi, ambapo historia inaonesha kuwa makombe ilikuwa ni biashara ya pili kwa ukubwa visiwani Zanzibar baada karafuu.

Bidhaa hii ilikuwa ikisafiriswa n’gambo kama vile nchi za Marekani, India na China na kuingizia nchi kipato. Kazi hii inaendelea kufanywa nchi nyingi duniani hadi sasa hasa katika nchi za visiwa kama yetu.

Na hivi sasa soko lake kubwa liko China ikifuatiwa na India, pia kwa hapa kwetu ni ajira kubwa kwa vijana wanaojishughulisha na utalii kwani watalii hununua bidhaa hiyo kama zawadi ya mapambo na kuondoka nayo.

Utalii wa Zanzibar ni tofauti na utalii wa nchi nyengine zenye mbuga za wanyama ikiwemo milima iliyotukuka, watalii hutoka makwao na kwenda huko kwa ajili ya kuangalia wanyama pori.

Lakini hapa kwetu watalii huja kwa kuvutiwa na historia ya nchi ambayo inakwenda sambamba na utamaduni wa asili wa watu wake kama vile mchanganyiko wa rangi tafauti za watu, upole ukarimu utulivu na upendo.

Pia kujionea mazingira ya fukwe safi za bahari na kupunga upepo mwanana uvumao kutoka bahari ya hindi ikiwemo mandhari ya kuvutia ya Mji Mkongwe pamoja na historia yake.

Pia hapa kwetu watalii hupata fursa ya kutembelea Kizimkazi na kwenda baharini ili kujionea samaki aina ya pomboo na kucheza nao. Kwa upande wa nchi kavu watalii hutembelea msitu wa Jozani na kujionea wanyama Kimapunju ambao ni adimu kuonekana sehemu nyengine duniani.

Haya yote niliyoyataja ni hazina kubwa ya nchi ambayo huipatia serikali fedha nyingi, maeneo haya pia kwa sehemu kubwa hutoa ajira kwa wananchi wanaojihusisha na sekta ya utalii.

Ukiacha Kimapunju waliopo msitu wa Jozani ambao ni adimu kuonekana sehemu nyengine ispokuwa Zanzibar, ndiyo hazina pekee Wazanzibari tulinayajua na tunaamini hivyo kuwa wanyama hao ni hazina ipekee tuliyo nayo kwa upande wa nyama.

Kumbe sivyo mambo yalivyo hatujafahamu tu. Ukweli ni kwamba wazanzibari temebarikiwa viumbe wengine wawili tena wa ajabu sana kwa wenzetu kwasababu hawapatikani makwao.

Viumbe hao ukiwataja au kuwaonesha katika ulimwengu wa Conchologist utaambiwa kwao ni Zanzibar kama walivyo Kimapunju.

Viumbe hao ni wawili ambao wana mnasaba na Zanzibar tu kwa maana ya kuwa huwezi kuwapata mahala pengine duniani. Kimoja kinaishi nchi kavu na chengine kinaishi baharini katika kina kirefu cha maji.

Viumbe hao ni aina ya ‘mollusks’. Hii ni hazina ya pili ya nchi ukitoa Kimapunju. Wanyama hao tutawaelezea na kuwa chambua katika makala zijazo.