KATIKA bara la Afrika, Tanzania ni moja kati ya nchi zinazosifika kwa kuwa na walimbwende wenye muonekano mzuri, sura na shepu za kuvutia.
Unapozungumzia warembo hao wakitanzania huachi kumtaja mwanadada aliyeiteka tasnia ya filamu nchini kwa umahiri wa kuigiza ambae anatambulika kwa jina la umaarufu ‘Lulu’.
Makala hii itakusimulia maisha ya mrembo huyu ambae amepata tuzo tofauti za filamu, ikiwemo ya Zanzibar International Film Festival kama msanii bora wa kike kupitia filamu ya ‘Foolish Age’ mnamo mwaka 2013.
Jina lake halisi ni Elizabeth Michael aliezaliwa Aprili 16, 1995 katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili jijini Dar Es Salaam Tanzania ambae ni mtoto wa Lucrecia Kalugira na Michael Kimemeta.
Alimaliza elimu ya msingi katika skuli ya Remnant Academy na Perfect Vision High School, St Mary’s High School alipata elimu yake ya sekondari.
Baadaye alijiunga katika Chuo Cha Utumishi Wa Umma Tanzania (TPSC) akisomea kozi ya stashahada ya Rasilimali Watu na Utawala.
Kipaji chake kilianza kujidhihirisha mapema mnamo mwaka 2000, wakati akiwa na umri wa miaka mitano na baadae alijiunga na kikundi cha Sanaa ‘Kaole Group’, ambapo aliigiza pamoja na waigizaji nguli nchini kama Vincent Kigosi na marehemu Steven Kanumba.
Jina la Lulu lilianza kutambulika wakati akiwa katika kundi hilo ambalo alilitumia katika tamthilia tofauti kama vile Gharika, Taswira na Zizimo, ambazo zilirushwa katika televisheni na kumpatia umaarufu hadi leo.
Wakati bado akiwa na umri mdogo Lulu alianza kujikita katika maigizo ya filamu, ambapo filamu yake ya kwanza ilikuwa ‘Misukosuko’ aliyoshirikiana na Jimmy Mponda.
Mnamo mwaka 2006, aliigiza filamu iitwayo ‘Wema’ iliyoandaliwa na ‘Game 1st Quality’ na badae filamu nyingine nyingi kama ‘Family Tears’, ‘Ripple of Tears’,’Passion’ na ’Dangerous Girl’, ambazo zimempatia umaarufu mkubwa na kutambulika sehemu nyingi ndani na nje ya Tanzania.
Pamoja na umri wake mdogo alionao Lulu, lakini mpaka sasa amepata kuigiza zaidi filamu ya 30.
Mbali na tamthilia na Filamu mbali mbali, pia amepata kufanya igizo la redioni lililoitwa ‘Wahapahapa’ ambalo alitumia jina la Mainda.
Igizo hilo liliandaliwa na Media For Development International wakishirikiana na Ubalozi wa Marekani,Wizara Ya Afya na Ustawi wa Jamii, pamoja na chuo cha ‘Johns Hopkins University Center For Communication Programs’ cha nchini Marekani.
Igizo hilo liliongozwa na Mmarekani anaefanya shughuli zake Afrika, Bwana Jordan Riber.
Aidha katika mradi huohuo wa ‘Wahapahapa’ alipata kuigiza katika video ya wimbo wa Lady Jay Dee uitwao ‘Shamba’ na wa Enika uitwao ‘Changanya’.
Lengo la kuanzishwa kwa mradi huo lilikuwa ni kuelimisha jamii juu ya malezi bora katika kipindi cha ukuaji wa mtoto.
Mnamo August 2013, Lulu alizindua filamu yake ya kwanza ambayo ameitaarisha yeye mwenyewe iitwayo ‘Foolish Age’.
Filamu hiyo ilizinduliwa katika ukumbi wa Mlimani City uliopo jijini Dar Es Salaam na kubahatika kuhudhuriwa na mamia ya watu.
‘Foolish Age’ ilifanya vizuri sokoni, ambayo ilipata nafasi ya kuoneshwa katika tamasha la kimataifa la filamu Zanzibar (Zanzibar International Film Festival ZIFF) na baadae kuteuliwa kuwania tuzo, ambapo Lulu alishinda tuzo ya muigizaji wa filamu wa kike anaependwa kupitia filamu hio katika ‘Tuzo za Watu’ mnamo mwaka 2014.
Mnamo mwaka 2015 alizindua filamu yake ya pili ambayo pia aliitayarisha yeye mwenye iitwayo ‘Mapenzi Ya Mungu’.
Filamu hio pia ilibahatika kuoneshwa katika tamasha la ZIFF, ambapo mwaka 2016 ilipata bahati ya kushinda filamu bora Afrika Mashariki, katika tuzo za ‘Africa Magic Viewer Choice Awards’ zilizofanyika Lagos nchini Nigeria.
Mnamo mwaka 2017, mrembo huyo ambae ni mweledi wa kuigiza, alitajwa kuwa ni miongoni mwa vijana 100 wa Afrika wenye ushawishi mkubwa katika Tuzo za Vijana wa Afrika zinazofanyika nchini Ghana.
Sio tu ana kipaji cha uigizaji, bali pia mrembo huyo amewahi Kuwa mtangazaji wa kipindi cha televisheni kiitwacho ‘Watoto Wetu’ Kilichorushwa na ITV Tanzania mnamo mwaka 2004-2007, wakati akiwa na umri mdogo.
Pia mnamo mwaka 2014 -2015 alikuwa mtangazaji wa mashindano ya kutafuta vipaji vya uigizaji Tanzania yaitwayo Tanzania Movie Talents (TMT).
Kutokana na ulimbwende na muonekano wa mrembo Lulu, mwenye mwili wa kibantu wenye shepu iliyogawika, ngozi laini yenye rangi ya kuvutia, sura nzuri na tabasamu mwanana, amekuwa ni kivutio na mfano wa kuigwa na warembo wengi.
Lulu amekuwa akiwavutia wengi kutokana na mavazi yake, mitindo ya nywele na hata makeup anazojipaka, ambapo miaka michache nyuma alivuta warembo wengi kwa aina ya wanja wake wa nyusi ambao wengi walianza kuuona kutoka kwake na Watanzania waliupa jina la wanja wa lulu.
“Hakika ni mrembo na mimi binafsi nampenda sana, hata kwenye simu yangu zimo picha zake nyingi na pia hupenda kuiga mitindo yake ya nguo” alisema Hudda Hassan mkaazi wa Kisauni wakati akifanyiwa mahojiano na mwandishi wa makala hii.
Unapotembelea salon nyingi Tanzania lazima utakutana na picha ya mrembo Lulu ambayo inaonesha mitindo yake ya nywele au hata make up.
Mwanaharusi Hemed ambae ni mwanadada anaemiliki saluni ya kike Kundemba mjini Unguja, alisema “Picha za Lulu zinavutia sana ukiweka kwenye saluni, na vile wengi wanampenda basi inakuwa ni moja ya matangazo yanayotusaidia kuonesha ubora wa huduma zetu”.
Kutokana na umaarufu wake pamoja na kupendwa na watu wengi ndani na nje ya Tanzania, makampuni mengi yamekuwa yakimtafuta Lulu kuwa balozi wa kushajihisha jamii juu ya jambo au bidhaa husika.
Mnamo mwaka 2013/14 alichaguliwa kuwa balozi wa tamasha la filamu liitwalo ‘Dar Film Festival’ lililofanyika Dar es Salaam.
Aidha mnamo mwaka 2015 alifanya kazi na kampuni ya simu ya Airtel Tanzania kama mtangazaji wa kipindi cha Airtel yatosha Tv Show.
Pia ni balozi wa kampuni ya Paisha Tanzania, inayojishughulisha na kufanya biashara mitandaoni na aliteuliwa na kampuni ya Hengan Baby Products and Sanitary co ltd Kuwa balozi wa freestyle napkins bidhaa za wanawake kwa miaka miwili.
Aidha Lulu ni balozi wa Sinema Zetu International Film Festival, ambalo ni tamasha la filamu linaloandaliwa na chaneli ya Sinema zetu ya kampuni ya Azam.
Pia ni balozi wa Azania inajulikana kama ‘Pishi la Lulu’, ni manager wa upcoming actor ajulikanae kama Suhelyht khan, ambae jina lake halisi ni Suhely Tarmohammed.
Kama waswahili wasemavyo kuwa maisha ni safari ndefu yenye mabonde na milima, maisha ya mrembo huyi yalikuja na hadithi mpya ya kusikitisha, ambapo mnamo Novemba 13, 2017, Lulu alishtakiwa kwa kosa la kuua bila kukusudia na alihukumiwa kifungo cha miaka miwili jela kwa kifo cha mwigizaji Steven Kanumba.
Alidaiwa kusababisha kifo cha Kanumba (aliekua na umri wa miaka 28), ambaye alikuwa akichumbiana naye wakati Lulu akiwa na umri wa miaka 17.
Lulu alikamatwa na kukaa rumande kwa takribani mwaka mzima kwa uchunguzi, baadaye mashtaka hayo yalibadilishwa na kuwa mauaji ya kukusudia.
Mnamo Mei, 2018 aliachiliwa kutoka gerezani na Mahakama Kuu ya Tanzania chini ya Sheria ya Huduma za Jamii ya 2002 na wakati uliobaki afanye huduma za jamii baada ya kuonyesha tabia nzuri wakati alipokuwa gerezani na mnamo Novemba 12, 2018 alikamilisha majaribio yake.
Mitihani na misukosuko aliyopitia ilikua ni moja ya funzo Kwenye maisha ya Lulu ambayo ilimsukuma katika masuala mazima ya uhisani na kusaidia wasiojiweza.
Mnamo Januari 23, 2019, Lulu alianza kampeni iliyoitwa “Save My Valentine” ambayo ililenga kukusanya pesa kwa kusaidia watu wenye mahitaji maalum.
Kupitia kampeni hiyo Lulu aliuza takribani nguo zake 62 na pesa zilizopatikana zilipelekwa kwenye baadhi ya vituo vya kulelea watoto yatima huko Iringa Tanzania wakati wa siku ya wapendanao.
Historia ya mrembo Lulu ambae bado ana umri mdogo amevuka milima na mabonde ya maisha, na licha ya changamoto na misukosuko aliyopitia, lakini bado amesimama imara na kuzitumia nyakati ngumu alizopitia kama ni moja ya funzo katika kukamilisha safari yake iliyobaki.
“Naamini jaribu lolote ni kama mbegu na sio tatizo kama wengi tunavyochukulia, kwani ukipanda mbegu sehemu kubwa ya shamba lako na mavuno yatakuja kwa ukubwa huo huo na ukipanda sehemu ndogo pia yatakuja kwa udogo huo, hivyo lilikua zito, kubwa, linaumiza zaidi ya ninachoweza kuelezea, lakini ninaimani lilikua ni mbegu” Lulu
MAKALA HII IMETAYARISHWA NA LAILA KEIS KWA MSAADA WA MTANDAO