NA HABIBA ZARALI, PEMBA

MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad amesema uadilifu na kujenga umoja ni ngazi muhimu itakayoifikisha Zanzibar na wananchi wake kwenye maslahi mapana na amani ya kweli.

Maalim Seif alieleza hayo huko katika skuli ya sekondari Uweleni, alipokuwa akizungumza na makundi maalum ya wananchi wa wilaya ya Mkoani ikiwa ni mara ya kwanza tangu ateuliwe kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais.

Alisema wakati umefika kwa wazanzibari wote kuwa wamoja wenye kufanya kazi kwa mashirikiano ili malengo ya serikali ya kukuza uchumi yaweze kufikiwa kwa maslahi ya wananchi wote.

Maalim Seif alisema Zanzibar bila ya maridhiano kati ya vyama vya siasa ni vigumu kupatikana kwa maendeleo hivyo maridhiano yaliyofikiwa yaungwe mkono ili Zanzibar ya maendeleo iweze kufikiwa.

“Nampongeza sana rais wetu Dk. Hussein Mwinyi kwa uamuzi wake wa kutaka maridhiano, kwani najua haikuwa rahisi kuungana kwetu, hata hivyo tumeunganishwa na maslahi ya Zanzibar na matakwa ya katiba yetu”, alisema.

Akizungumzia kuhusu uadilifu kwa viongozi waliochaguliwa na kuteuliwa, Makamu huyo alisema wana wajibu wa kutoa huduma sawa kwa wananchi bila ya ubaguzi, ili lengo na dhamira ya viongozi kuwaunganisha wazanzibari liweze kutimia.

Makamu huyo aliwataka wananchi hao kuacha tofauti zao za kisiasa kwani ndizo zinazoleta mifarakano na badala yake waungane kwa kuleta maendeleo ya wazanzibari.

“Mimi na Rais Mwinyi tunafanya kazi kwa pamoja kama katiba yetu inavyotutaka na niwahakikishie katika serikali hii ya awamu ya nane hayatotokea maovu kwani viongozi tuko makini”, alisema.

Alifahamisha kuwa wazanzibari wote ni wamoja na wenye maslahi ya hatma ya Zanzibar na hakuna haja ya kuleta malumbano kwani kufanya hivyo kunaipotezea hadhi nchi na wananchi wote.

Mapema akimkaribisha Makamu wa Kwanza wa Rais, Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba, Mattar Zahor Masoud aliwataka wananchi kuunga mkono maridhiano waliyoyafikia na viongozi wao na ili nchi iweze kuwa kwenye amani na kufikiwa maendeleo.

Alisema umoja ndio silaha ya mafanikio kwa wananchi na taifa lolote hivyo kila mmoja ana haki na wajibu wa kuona nchi inapiga hatua za haraka za maendeleo.

“Viongozi wetu tayari wameshaonesha nia na dhamira njema kwetu sisi wazanzibari ni wajibu wetu sasa kuungana nao”, alisema.

Wakitoa shukrani zao wananchi hao waliipongeza serikali ya awamu ya nane kwa kuondoa chuki, visasi na mifarakano miongoni mwa wazanzibari.

Wananchi hao waliahidi kushirikiana pamoja na serikali kwa maslahi mapana ya Zanzibar na watu wake na kuweka mbali itikadi zao za kisiasa.

Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, anatarajiwa kufanya ziara kama hiyo katika wilaya zote Unguja na Pemba.