TUNIS,TUNISIA

VIJANA wenye hasira wameendelea kukaidi amri ya karantini ya nchi nzima huko Tunisia hasa nyakati za usiku na wameendelea kufanya maandamano licha ya kuweko maambukizi ya kirusi cha corona.

Kwa mujibu wa shirika la habari la IRIB, waandamanaji walimiminika katika mitaa ya Tunis, mji mkuu wa Tunisia na miji mengine kama Sousse, Kasserine, al Mahdia, al Monastir na miji mengine kadhaa na kupambana na polisi.

Baadhi ya vyombo vya habari vilisema kuwa, vijana hao wa Tunisia wanalalamika kutoona mabadiliko yoyote ya maana tangu baada ya kutokea mapinduzi ya wananchi miaka kumi iliyopita.

Maandamano hayo aidha yanatokana na malalamiko ya vijana wa Tunisia wanaolalamikia matatizo ya kiuchumi na kijamii yanayotokana na kutokuweko utulivu wa kisiasa nchini humo ambao hivi karibuni ulilazimisha kubadilishwa Baraza la Mawaziri.

Sababu nyengine ni matatizo mengi yaliyosababishwa na ugonjwa wa corona.

Askari wa kulinda usalama walitumia gesi za kutoa machozi kuwatawanya waandamaji waliokuwa wakiwalenga kwa mawe askari hao,kufunga barabara na kuwasha moto majiani.

Huku hayo yakiripotiwa, wizara ya ulinzi ya Tunisia ilisema kuwa,jeshi litatumwa katika miji ya nchi hiyo kwa ajili ya kuwasaidia polisi kukabiliana na vijana wanaofanya fujo hasa katika miji ya Siliana, Kasserine, Sousse na Bizerte.

Miji mengine iliyoshuhudia maandamano ya vijana hao ni pamoja na Kairuoa, Kebili, Nabeul na Manouba Gafsa.

Wizara ya mambo ya ndani ya Tunisia ilisema, karibu watu 1,000 walitiwa mbaroni hadi hivi sasa kwa kushiriki katika maandamano hayo ya fujo.