NA JOSEPH NGILISHO, ARUSHA

WAMILIKI na Madereva wa magari ya kukodisha Mkoani Arusha, wameiomba serikali kupitia Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, kuangalia upya ada ya sh, milioni  1  iliyopendekezwa kwa mwaka kwenye magari hayo kwa lengo la kuwezesha watoa huduma kuendelea kufanya biashara zao.

Wakitoa maoni yao jana kwenye kikao cha kujadili ada hiyo jana Jijini Arusha, wadau hao wameiomba serikali kupunguza kiwango cha ada hiyo na kufanya utafitu wa kina, ili kuja na bei halisi ya tozo za magari hayo.

Brian Fadhil, alisema ada iliyopendekezwa ni kubwa sana kulingana na aina ya biashara wanayofanya hivyo ni vyema suala hilo likaangaliwa kwa kina na kabla ya kufanya utafiti wangeshirikisha wadau ili kuja na bei ya chini.

“Ni heri ada ikawa sh, 200,000 au hata sh,75000 kwa gari moja badala ya sh, milioni 1, sasa hivi biashara hakuna unaweza kukaa hata miezi miwili hujakodishwa gari lako”

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Kutetea Abiria (Akiboa) Locken Massawe, alisema wasafirishaji wanapaswa kujenga hoja ambazo zitaifanya serikali kufanya maamuzi ya kupunguza au kubakiza ada hiyo.

“Hoja tutakazojenga hapa ndio zitaamua kupunguza au kubakiza ada hiyo kwani serikali ni sikivu na inafanya maamuzi kwa kuzingatia maoni na ndio maana wanaamua ada hii ibaki kama ilivyo au la” 

Pia aliiomba wizara hiyo izungumze na halmashauri ya miji na majiji, ili kutenga maeneo maalum ambayo magari ya kukodisha yanaweza kupatikana ili kurahisisha watumiaji wa huduma hiyo.

Ambapo Meneja Leseni kutoka Mamlaka ya Udhibiri wa Usafiri Ardhini (LATRa), Leo Ngowi alisema nia ya mamlaka hiyo kuitisha mkutano huo  ni kusikiliza maoni ya wadau hao na kuboresha huduma za usafirishaji nchini

Awali Mhandisi ,Aroni Kisaka Mkurugenzi Idara ya Uchukuzi alisema mamlaka hiyo imepokea maoni hayo na itayafanyia kazi kwa kuyawasilisha mamlaka husika, ili serikali kupanga bei moja kwa wadau hao wa usafirishaji.