NA AHMED MAHMOUD ARUSHA 

SERIKALI imeiagiza halmashauri ya jiji la Arusha, kuhakikisha Madiwani wanakuwa na kalenda ya vikao, ili waweze kutoa taarifa kwa wananchi kuhusu utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwenye kata zao.

Agizo hilo limetolewa na Mkuu wa mkoa wa Arusha, Idd Kimanta, alipokuwa akifungua semina elekezi ya siku tatu ya madiwani inayofanyika ukumbi wa halmashauri ya jiji, kwa ajili ya kuwajengea uelewa wa majukumu na mipaka yao ili kuondoa muingiliano kati yao na watendaji wa halmashauri hiyo.

Amesema ni lazima halmashauri iwe na vikao vya kikanuni na hatarajii kusikia vikao havifanyiki kwa kuwa lengo la vikao hivyo ni kuwawezesha madiwani  kuwa na taarifa ya miradi inayotekelezwa kwenye maeneo yao na hivyo kuwawezesha kuisimamia kulingana na fedha zilizotolewa na serikali.

Kimanta, amesema baada ya semina hiyo  madiwani watakuwa wameelewa mipaka ya majukumu yao hivyo hakutakuwepo na migogoro kati yao na watendaji.

 Amewataka wakuu wa Wilaya Mkoani humo, kuhakikisha wanasikiliza kero zilizopo kwenye wilaya zao na wakishindwa kuzipatia ufumbuzi ndipo waziwasilishe kwake kila mkuu wa wilaya na wahakikishe maeneo yao yapo salama.

Kuhusu usafi amesema anakerwa na uchafu  unaoufanya mji huo kuwa mchafu ,akitolea mfano eneo la kituo kikuu cha mabasi yaendayo mikoani jijini Arusha,ambalo kumekithiri uchafu hasa nyakati za usiku.

Kimanta, amesema   kuna uchafu na taka nyingi zinazozalishwa na kuchafua taswira ya kituo hicho cha mabasi hivyo akaiagiza halmashauri ya jiji kuchukua sheria ili kuwadhibiti wanaochafua maeneo hayo.

Amewataka Madiwani kuhakikisha swala la ongezeko la watoto wa mitaani, linazibitiwa na ameshangazwa na ongezeko la watoto hao na kuhoji wanatoka wapi .

Kuhusu kelele zinazotokana na matangazo ya wajasiriamali wanao weka vipaza sauti (Speker) vya matangazo ya biashara , kwenye maduka na maeneo mengine ya biashara kwa ajili ya kuvutia wateja wao amesema  kelele hizo zimezidi na ni nyingi zimekuwa ni kero.

 Hivyo akaitaka halmashauri kutumia sheria ili kelele hizo ziishe na wanaofanya biashara zao wafanye bila kelele na kusisitiza kwamba anataka Arusha iliyotulia.

 Kwa upande wake mstahiki Meya Maxmiliani Ilanqe, amesema jiji limejipanga kwa ajili ya kukusanya mapato pamoja na swala la usafi wa jiji hilo ambalo lilibatizwa kuwa ni  Geneva ya afrika .

Amewataka wataalamu wa halmashauri hiyo  kukaa mkao wa mguu sawa kwa ajili ya kuwajibika kila mmoja kwenye eneo lake na madiwani watashikamana pamoja kuhakikisha usafi na mapato ya halmashauri yanaongezeka na kuboresha jiji hilo liwe ni mfano wa majiji yanaoyoongoza kwa utalii ulimwenguni.

Amesema dhamira yake ni kulifanya jiji liwe linaongoza kwa usafi nchini katika kipindi chote cha uongozi wake ,kwa mapato na usafi, na kuwaomba wananchi walipe kodi za halmashauri hiyo kwa hiari wasisubiri kusukumwa.

 Mkurugenzi wa jiji Dakta John Pima, alisema Julai mwaka huu jiji litaweka Vikapu au mapipa ya kutupia taka maeneo mbalimbali ikiwa ni hatua ya kuimarisha usafi na kuliweka katika mazingira ya muonekano wa jiji lenye  ubora.

Alisema kuwa kwenye bajeti ijayo wanakusudia kuweka mapipa kila eneo kwa ajili ya kuwezesha wananchi kutupa taka na kutokuchafua mji.