MAPUTO, MSUMBIJI
KIMBUNGA Eloise kimesababisha maelfu ya watu kuachwa bila makaazi nchini Msumbuji.
Kwa mujibu wa taarifa kimbunga hicho kilicholeta upepo wa kasi ya kilomita 150 kilisababisha mvua na mafuriko katika mkoa wa Sofala katika pwani ya Msumbuji.
Idara ya Kitaifa ya Kukabiliana na Maafa nchini Msumbiji ilisema watu wapatao 6,859 waliachwa bila makaazi kufuatia kimbunga hicho hasa katika wilaya ya Buzi.
Mashirika ya kutoa misaada yalisema yanahitaji misaada ya dharura ya chakula, maji ya kunywa na makaazi ya muda kwa walioathirika.
Aidha imekuwa vigumu kuwafikia baadhi ya watu walioathirika katika wilaya ya Buzi kutokana na mafuriko ambayo yalifunga njia zote za mawasiliano.
Kimbunge Eloise pia kiliharibu hekari 136,755 za mashamba mbali na kuharibu kabisa skuli nane na kusababisha uharibufu mdogo katika skuli nyengine 17 na hospitali 11.
Hali kadhalika nyumba zaidi ya 1000 ziliharibiwa kabisa na kimbunga hicho.
Taarifa zilisema kimbunga hicho pia kilisababisha mvua kubwa katika nchi jirani za Zimbabwe, Afrika Kusini na Eswatini.
Mwaka 2019 Msumbuji ilikumbwa na vimbunga viwili Idai na Kenneth ambapo idadi kubwa ya watu walipoteza maisha na miundombinu muhimu kuharibiwa huku makumi ya maelfu wakiachwa bila makaazi.