NA KHAMISUU ABDALLAH

SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar kupitia idara ya Mipango Miji na Vijiji imeombwa kuyahifadhi maeneo ya wazi yaliyobaki hasa katika maeneo ya Mjini, ili yasiendelee kuhujumiwa.

Ombi hilo limetolewa na Meneja wa kitengo cha maradhi yasioambukiza kutoka Wizara ya Afya Omar Abdalla Ali wakati akizungumza na Zanzibar leo ofisini kwake Mnazimmoja.

Alisema maeneo mengi yaliyokuwa ya wazi hivi sasa yanajengwa kwa kasi hali ambayo inawakosesha fursa wananchi za kufanya mazoezi.

Aidha alisema zamani kulikuwa na maeneo mengi ya wazi lakini hivi sasa mengi yao yamegeuza nyumba za makaazi na maduka.

“Mjini kulikuwa na maeneo mengi ya wazi na vyoo lakini hivi sasa yamegeuzwa maduka ya kuuza vifaa mbalimbali ikiwemo vya skuli,” alisema.

Akiyataja maeneo hayo alisema ni pamoja na Kombawapya, Mapembeani, Malindi kibandamaiti huku vyoo vilivyokuwepo ni pamoja na Saateni, Kinazini, Miembeni, Weles, Malindi, Makadara na vyenginevyo.        

Meneja huyo alifahamisha kwamba zamani kulikuwa na maeneo mengi ya wazi ambayo yaliwapa fursa wananchi kufanya mazoezi wakati wote.

Alisisitiza kuwa ni vyema kwa idara hiyo kuchukua jitihada za kuyahifadhi maeneo hayo kwa vizazi vya sasa na baadae.

Alisema hivi sasa watu wengi hawafanyi mazoezi kutokana na kukosa maeneo ya kufanyia mazoezi hali ambayo inapekea kupata maradhi yasioambukiza.

Alibainisha kwamba Zanzibar ina sheria na kanuni nzuri lakini utekelezaji wake sio mzuri.

Sambamba na hayo aliiomba serikali kutengeneza bajeti maalum kwa ajili ya kuweka njia za watu wanaokwenda kwa miguu ili kuepusha ajali zisizokuwa za lazima.

Aidha alisema kuwepo kwa njia hizo pia itatoa fursa kwa wananchi kupata nafasi ya kufanya mazoezi ya viungo ili kujikinga na maradhi mbalimbali.

Nao, wananchi mbalimbali wakizugumza na gazeti hili walisema ukata wa vyoo linawapa tabu kubwa hali ambayo inapelekea watu wengi kumwaga kinyesi ovyo na kuharibu mazingira.

Issa Mselem alisema maeneo mengi ya Mjini yalikuwa na vyoo vya serikali lakini hivi sasa havipo.

“Ukienda Mnazimmoja kuna choo kimoja tu ambacho unatakiwa ulipie shilingi 500 ukiachia kile cha uwanjani cha bure lakini muda wote unavikuta vimefungwa,” alisema.

Nae Salma Khamis aliiomba serikali kurejesha vyoo katika maeneo ambayo yaliwekwa maalum kwa ajili ya huduma hiyo ili kuepusha watu kuharibu mazingira.