NA TATU MAKAME

CHUO cha Mafunzo Zanzibar kimeeleza kuwa kimejipanga kuongeza idadi ya ng’ombe wa maziwa watakaofugwa katika vituo mbali mbali vya chuo hicho kuimarisha uzalishaji.

Kamishna wa Chuo cha Mafunzo Zanzibar, Ali Abdalla Ali, alisema hayo ofisini kwake Kilimani wakati alipozungumza na Zanzibar leo na kueleza kuwa wanatarajia kuongeza ng’ombe 10 kutoka wawili wa awali kwa lengo la kuongeza uzalishaji wa maziwa na kusaidia kuchangia pato la serikali.

Alisema kuongezeka kwa wanyama hao kikosi hicho kitaweza kutoa huduma ndogondogo katika kambi mbalimbali za chuo hicho.

“Kama hatuongezi mbinu za uzalishaji, tutategemea ruzuku serikalini hadi lini. Inavyotakiwa na sisi tujiongeze,” alisema.

Alibainisha kwamba ng’ombe hao watakapozalisha watachangia pato la serikali kwa kupeleka kima watakachopangiwa na serikali kuu ambacho kitaongeza pato la taifa.

“Mwaka 2020 tulitakiwa kuchangia serikalini shilingi Milioni 60 na tulipeleka Milioni 45 ingawa kima tulichopangiwa hakikutimia lakini fedha hizo sio kidogo,” alibainisha.

Kuhusu vituo ambavyo vitafugwa ng’ombe hao ni pamoja na Kangagani, Hanyegwa Mchana, Kiromoshi na maeneo mengine hivyo alisema wanamifugo mengine kama ngombe wa kienyeji, mbuzi na kuku ambao wanasaidia kuongeza uzalishaji katika kambi zao.