BAMAKO, MALI

JESHI la Mali limesema operesheni ya pamoja kati ya askari wa nchi hiyo na Ufaransa ndani ya siku chache zilizopita imepelekea kuuawa takribani wanachama 100 wa magenge ya kigaidi katikati ya nchi.

Taarifa ya jeshi hilo ilisema, mbali ya baadhi yao kuangamizwa katika operesheni hiyo iliyofanyika kati ya Januari 2 na 20, magaidi wengine wasiopungua 20 wametiwa mbaroni.

Taarifa hiyo iliongeza kuwa, lengo la operesheni hiyo lilikuwa ni kuwafurusha wanamgambo hao katika maficho yao yaliyoko katika maeneo ya karibu na mpaka wa nchi hiyo na Burkina Faso.

Kwa mujibu wa taarifa, magenge hayo ya kigaidi yenye kushirikiana na mtandao wa al-Qaeda pamoja na kundi la kigaidi la ISIS, yanadhibiti sehemu kubwa ya maeneo ya katikati mwa Mali.

Hivyo yamekuwa yakiendesha mashambulizi yao kutokea maeneo hayo.

Mali imo kwenye machafuko tangu mwaka 2012, baada ya wanajeshi kufanya mapinduzi katika nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.

Mnamo mwaka 2013 Umoja wa Mataifa ulituma kikosi cha askari wa kimataifa cha MINUSMA nchini Mali, kwa ajili ya kukabiliana na waasi pamoja na wanamgambo hao kikishirikiana na wanajeshi wa Ufaransa.

Hata hivyo askari hao wa UN na wa Ufaransa hawajafanikiwa kurejesha amani na utulivu nchini Mali, ambapo nchi hiyo bado inakabiliwa na tishio kubwa la makundi ya kigaidi yanayofanya mauaji ya mara kwa mara.