TOKYO, JAPANI
MAHAKAMA ya eneo la Tokyo imetoa uamuzi unaosema kuwa sheria ya Japani inayozuia mtu kuwa na uraia wa nchi mbili haikinzani na katiba.
Sheria ya Uraia ya Japani inaeleza kuwa raia wa Japani watapoteza uraia wao ikiwa watapata uraia wa nchi nyengine kwa hiari yao wenyewe.
Kesi hiyo iliwasilishwa mahakamani na watu sita waliopoteza uraia wa Japani baada ya kupata wa Uswizi na Liechtenstein walikohamia.
Walalamikaji walitaka serikali ithibitishe uraia wao wa Japani, wakisema kuwa kukataa kutambua uraia wa nchi mbili kunakiuka katiba ya Japani.
Katika uamuzi wao jaji kiongozi wa Mahakama ya Eneo la Tokyo, Mori Hideaki, alikataa madai ya walalamikaji hao.
Alisema ingawa katiba inawapa watu wote uhuru wa kuhamia nchi za kigeni na kubadilisha utaifa wao wa Japani, haisemi chochote juu ya haki ya kuendelea kubakia na uraia wa Japani katika hali kama hizo.