NA KIJA ELIAS, MOSHI
WAKATI Mahakama nchini ikijiendelea kuadhimisha wiki ya sheria ambayo inambatana na maadhimisho ya miaka 100 ya huduma ya mahakama, Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Moshi, Beatrice Mutungi, ameishauri serikali kuhakikisha kwamba maeneo ya kihistoria yaliyokuwa yakitumiwa na Mahakama yanahifadhiwa kwa ajili ya vizazi vijavyo.
Akizungumza jana kwenye wiki ya sheria katika viwanja vya Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi Jaji Mutungi, amesema kuna maeneo ya kihistoria ya mahakama ambayo yalitumika enzi za utawala wa machifu, ikiwemo kitanzi kilichopo maeneo ya Wold CCM, kimevamiwa na wananchi na kujenga maeneo ya biashara.
Jaji Mutungi alisema serikali haina budi kuyahifadhi maeneo ya Mahakama ambayo yalikuwa yakitumika enzi za utawala wa machifu, hali ambayo itawawezesha wananchi kujua historia na kwamba watakuwa na utamaduni wa kuyatembelea maeneo hayo na kujua historia yake.
“Tunayo maeneo ya kihistoria ukiwemo mti mkubwa ambao ulikuwa ukitumika kunyongea watuhumiwa, ambao unapatikana katika mahakama ya mwanzo Wold Moshi, Jiwe au kiti cha kuhukumia ambacho kipo katika mahakama ya mwanzo Marangu, majengo ya kihistoria ya mahakama za mwanzo Kibosho, Kindi na Uru, maeneo haya yote yamehifadhiwa,”alisema Jaji Mutungi.
Amesema wiki ya sheria ambayo inaambatana na maadhimisho ya miaka 100 ya huduma ya mahakama ni vizuri wananchi wa Mkoa wa Kilimanjaro kutembelea sehemu za kihistoria yaliyopo katika mkoa huo ili kujifunza historia ya nchi yao na kutuza utamaduni iliopo.
Aidha, Jaji Mutungi, amesema makahaka kwa kushirikiana na wadau wake wamelenga kuitumia kwa ajili ya kutoa elimu ya kwa wananchi juu ya masuala mbalimbali ya kisheria, utendaji kazi wa mahakama kwa kushirikiana na wadau lengo likiwa ni kuwahudumia wananchi wote watakaojitokeza.
Aliongeza kuwa “Kumekuwepo na mabadiliko makubwa katika suala zima la utoaji haki hili limechangiwa na kuwepo kwa maboresho mbalimbali yanayofanywa na mahakama katika kuhakikisha haki inapatikana kwa wote na kwa wakati,”alisema.
Kwa upande wake Afisa Tehama Mahakama Kuu Moshi, Benjamin Mhume, amesema kuanzishwa kwa mfumo wa video cout, hadi sasa wamefanikiwa kusikiliza kesi 15 kutoka nje ya nchi na kesi hizo zimesikilizwa na kutolewa maamuzi.
“Kuwepo kwa teknolojia hii imepunguza gharama za shahidi pamoja na watuhumiwa kusafirishwa kwa ajili ya kwenda kusikiliza kesi zao mahakamani,”alisema.
Awali akizindua wiki ya sheria Mkuu wa wilaya ya Moshi Alhaji Rajab Kundya, aliwataka wananchi kutumia fursa waliyopewa na mahakama kupata ushauri, elimu na msaada wa kisheria kupitia taasisi zitakazoshiriki ambazo zimejitolea kutoa huduma hiyo kwenye maadhimisho hayo.
“Elimu ya kisheria watakayoipata itawawezesha kuzitambua haki zao na kuifahamu sheria, taratibu za kimahakama au kwa kuwasuluhisha katika masuala ambayo yatakuwa hayana umuhimuwa kufika mahakamani, jambo ambalo litapunguza muda mwingi na gharama zitakazotumika kuhudhuria mahakamani, kuondoa migogoro katika jamii na kujenga jamii yenye amani, mshikamano na kukuza ustawi wa wananchi,”alisema.
Maadhimisho ya wiki ya Sheria yamebeba Kauli Mbiu ya “Miaka 100 ya Mahakama Kuu;Mchango wa mahakama katika kujenga Nchi inayozingatia Uhuru, Haki, Udugu, Amani na Ustawi wa Wananchi 1921-2021.”