NA MARYAM HASSAN.

MMOJA ya majeruhi wa ajali ya kuanguka kwa jengo la Beit el Ajaib, aliyekuwa amelazwa katika chumba cha uangalizi maalum (ICU) anaendelea vizuri baada ya kutolewa katika chumba hicho na kuwekwa katika wodi ya kawaida.

Akizungumza na Zanzibar Leo, Msemaji wa Hospitali kuu ya Mnazi Mmoja, Hassan Makame Mcha, alisema mgonjwa huyo hivi sasa anaendelea vizuri huku madaktari wakisubiri apone kidonda cha mguu uliokatwa ili afanyiwe matibabu mguu mwengine.

Majeruhi huyo Dhamir Salum Dhamir (37) mkaazi wa Kinuni, wilaya ya Magharibi ‘B’, aliumia miguu yote miwili na kupelekea kukatwa mguu mmoja ambao ulikuwa umeathirika zaidi.

Alisema kwa mujibu wa taarifa za daktari mgonjwa huyo hawezi kufanyiwa upasuaji wa mguu wa pili kabla ya kupona kwa kidonda cha mguu wa mwanzo hivyo anaendelea kupatiwa matibabu.

“Kwa sasa hali yake inaendelea vizuri kwa sababu madaktari wapo karibu sana na mgonjwa huyo kwa ajili ya kumpatia matibabu,” aliongeza Mcha.

Kwa upande wa majeruhi mwengine, Hamad Matar aliyevunjika mkono wa kushoto na kupelekea kuondolewa kwa baadhi ya vidole vya mkono wake alisema anaendelea vyema ingawa bado yupo katika uangalizi wa karibu wa madaktari.

“Kwa ujumla hali zao mpaka sasa zinaleta matumaini tofauti na walivyoletwa awali lakini bado wapo chini ya uangalizi wa madaktari wetu” alisema.

Tukio la kuporomoka kwa jengo hilo la kihistoria lilitokea Disemba 25 mwaka uliopita ambapo mbali ya majeruhi hao, watu wawili walifariki dunia huku serikali ikiunda kamati ya wataalamu kuchunguza chanzo cha ajali hiyo.