NA ZAINAB ATUPAE

WAJUMBE wa Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Soka Zanzibar ZFF wamemkataa Makamu wa Rais wa Shirikisho hilo Salum Ubwa kutoendelea kushikilia wadhifa huo.

Ubwa alikataliwa kwa kupigiwa kura za hapana 14 na kura 11 ndio zilizomkubali kati ya kura 25 katika mkutano huo uliofanywa Kilimani.

Aidha wajumbe hao walimrejesha na kuendelea kuwa rais wa Shirikisho hilo kwa kumpigia kura 21 za ndio na kura tatu zilimkataa na moja iliharibika.

Wajumbe hao walipiga kura za kuwakubali au kumkataa kuendelea kuwa viongozi wa Shirikisho hilo kwa kupiga kura za siri.

Utaratibu wa kupigwa kura hizo ambazo zilisimamiwa na Mrajisi wa vyama vya Michezo Zanzibar Suleiman Kweleza ambapo kabla ya kupigiwa kura alitolewa nje na kuanza kuwahoji mmoja mmoja na kupigiwa kura.

Sambamba na hao wajumbe hao waliweza kuwa na imani na wajumbe wote wa Kamati tendaji ya Shirikisho hilo.

Wajumbe hao ni Ali Mohammed Ameir, Nasra Juma, Kibabu Haji Hassan, Seif Mohammed, Omar Ahmed na Salum Ali Haji.

Aidha baada ya uchaguzi huo wajumbe walitoa maazimio ambayo waliitaka kamati hiyo kuyafanyia kazi,ili  kuendeleza soka lao.

 Baadhi ya maazimio hayo ni pamoja na rais wa Shirikisho hilo kupata nafasi ya kuchagua makamu wa rais, wajumbe wa mkutano mkuu kuchaguliwa kwenye mikoa yao, rais kupewa nafasi ya kuchagua wajumbe wanne badala ya wawili aliokuwa akichagua hapo awali,katiba kubadilisha lugha kutoka ya kiengereza kuwa ya kiswahili, kuwepo katibu msaidizi  kutoka Pemba.