TUCHUKUE fursa hii kuwapongeza makatibu wakuu na manaibu makatibu wakuu wa wizara ya serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar walioteuliwa na kuapishwa hivi karibuni.

Makatibu wakuu na wasaidizi wao ni watendaji na wasimamizi wajukumu ya serikali katika wizara, ambazo kwa kawaida huwa na idara na taasisi kadhaa.

Tunaposema watendaji na wasimamizi wakuu tunamaanisha ndio wanaopaswa kuhakisha haki na wajibu wa watendaji wa chini walio kwenye wizara yake vinatekelezwa.

Aidha makatibu na wasaidizi wao ndio wanaopaswa kusimamia matumizi na makusanyo ya fedha za serikali na kuhakikisha yanatumika sawa kulingana na bajeti lakini pia kuhakikisha wanakusanya fedha.

Tunaelewa vyema kwenye hafla ya kuapishwa kwa makatibu, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi amemaliza maneno yote, hata hivyo kama binaadamu wakati mwengine tunapaswa kukumbusheni.

Serikali ya awamu ya nane ambayo tangu iingie madarakani ina miezi karibu mitatu, imeanza na kasi kubwa katika nyanja zote, huku ikisimama kidete katika kukabiliana na changamoto zilizokuwa zikiwakabili wananchi kwa muda mrefu sana.

Moja ya changamoto iliyopo ni rushwa ambapo tunadiriki kusema kuwa tatizo hili lipo hata kwenye idara na taasisi za umma, hivyo makatibu wakuu ni jukumu lenu kuhakikisha tatizo hilo ambalo linamchukiza Rais wetu na wananchi linakomeshwa.

Zipo idara na taasisi baadhi ya wafanyakazi ambao wameshahudumu makazini kwa zaidi ya miaka 10 lakini kwa bahati mbaya hawajawahi kuisikia wala kuiona na wala hawajui kama kuna fedha wanayopaswa kulipwa wakati wa likizo.

Wapo wengine wanafanyakazi kwa moyo mmoja bila kuchoka na siku zote wanatumia zaidi muda wao kazini, lakini kwa bahati mbaya wanacholipwa hakiwiani na kazi kubwa wanayoifanya.

Wapo wakuu wa idara na taasisi wanauzito wa kusimamia maslahi ya wafanyakazi wao wa chini, hivyo kila siku malalamiko kwenye taasisi hizo hayeshi.

Aidha wapo wafanyakazi wa chini watoro makazini haweshi dharura kwa maana ya kwamba hamalizi wiki kazini bila ya dharura, wapo wasiowajibika ambao wanakwenda na kurudi kazini ukimuuliza kafanyakazi gani hana alilolifanya.