NA MARYAM HASSAN

LESENI ya njia imemponza mshitakiwa Mtwana Vuai Mtwana (30) mkaazi wa Mtopepo, jambo lililopelekea kutozwa faini ya shilingi 100,000 na Hakimu wa mahakama ya mwanzo Mwera.

Mbali na kosa hilo, pia mshitakiwa huyo amesomwa kosa la kuendesha chombo kikiwa hakina bima, kinyume na kifungu cha 3 (1) (2) sura ya 136 sheria za bima Zanzibar.

Hakimu wa mahakama hiyo, alimtaka mshitakiwa huyo kwa kila kosa kulipia faini ya shilingi 50,000 na akishindwa atumikie Chuo cha Mafunzo kwa muda wa wiki tatu.

Kabla ya kupewa adhabu hiyo, Mwendesha Mashitaka kutoka jeshi la Polisi, Koplo Khadija Abdalla, alidai kuwa mshitakiwa alipatikana na kosa hilo Januari 17 mwaka huu, majira ya saa 4:30 za asubuhi huko Dongongwe wilaya ya Kati mkoa wa Kuwini Unguja.

Mshitakiwa alipatikana akiwa anendesha pikipiki yenye nambari za usajili Z 291 HT akitokea Mchangani kuelekea Ndagaa, ikiwa honda hiyo haina leseni ya njia jambo ambalo ni kosa kishera.

Aidha Mwendesha Mashitaka huyo alisema, honda hiyo alikuwa akiendesha ikiwa haina bima jambo ambalo ni kosa kisheia.

Baada ya kusomewa mashitaka yake mshitakiwa alikubali na kuiomba mahakama kumpunguzia adhabu, kwa kuwa ndio kosa lake la mwanzo kufikishwa mahakamani.

Hakimu Johari Ali Makame wa mahakama ya mwanzo Mwera, alimtaka mshitakiwa kwa kila kosa alipe faini ya shilingi 50,000 na akishindwa atumikie Chuo cha Mafunzo kwa muda wa wiki tatu.

Mshitakiwa amelipa faini hiyo na kujinusuru kutumia adhabu aliyopewa na mahakama.