NA MARYAM HASSAN

MKAAZI wa Mwera Pongwe, amepelekwa rumande baada ya kunyimwa dhamana na mahakama ya mkoa Mwera.

Mkaazi huyo ni Suhaibu Issa Ibarahim (20) mkaazi wa Mwera Pongwe Unguja, ambae alifikishwa mahakamani hapo kwa kosa la kubaka na kutorosha mtoto wa kike aliyechini ya uangalizi wa wazazi wake, jambo ambalo ni kosa kisheria.

Suhaibu alipanda mahakamani hapo mbele ya Hakimu Khamis Ali Simai na kusomewa shiataka lake na wakili wa serikali, kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Sara Omar Hafidh.

Akisoma hati hiyo, wakili Sara alisema kuwa mshitakiwa alitenda kosa hilo Febuari 7 mwaka jana saa 2:15 usiku,  huko Mwera Pongwe wilaya ya Kati mkoa wa Kusini Unguja.

Alisema bila ya halali, alimchukua mtoto wa kike mwenye umri wa miaka 16 ambaye yupo chini ya uangalizi wa wazazi wake na ambae hajaolewa, kutoka njiani  na kumpeleka kwenye nyumba huko huko Mwera Pongwe.

Aidha inadaiwa kuwa mshitakiwa huyo, pia alimungilia kimwili (kubaka) majira ya saa 4:15 usiku huko Mwera Pongwe, jambo ambalo ni kosa kisheria.

Aliposomewa shitaka lake mshitakiwa huyo alikataa nakuomba kupewa dhamana, jambo ambalo lilikataliwa. Hakimu Khamis alisema mahakama hiyo haina uwezo wa kutoa dhamana kwa makosa ya aina hiyo, hivyo mshitakiwa aliamuru apelekwe rumande hadi Januari 20 mwaka huu