BAMAKO,MALI

UONGOZI nchini Mali umewafungulia mashitaka watu sita mashuhuri akiwemo waziri mkuu wa zamani Boubou Cisse, kwa kutaka kufanya mapinduzi.

Mawakili wao walisema hatua hiyo ilitokea baada ya njama ya jeshi kuipindua serikali mwezi Agosti.

Kulingana na mwendesha mashitaka watano kati ya watu hao sita walizuiliwa na polisi kwa sasa isipokuwa Cisse ambaye hajulikani alipo.

Taarifa za ndani kuhusiana na njama ya watu hao sita bado hazijulikani ila yote haya yanatokea wakati ambapo kuna msukosuko nchini humo kufuatia kuondolewa madarakani kwa Rais aliyechaguliwa Ibrahim Boubacar Keita na wanajeshi mnamo Agosti 18.

Kutokana na kitisho cha vikwazo vya kimataifa, jeshi la nchi hiyo lilikabidhi madaraka kwa taasisi ya mpito itakayodumu kwa miezi 18 kabla kufanyika kwa uchaguzi.