NA ABOUD MAHMOUD

KOCHA mkuu wa timu ya soka Malindi Mohammed Badru Juma, amesema licha ya kuwa nafasi za chini, katika msimamo wa ligi kuu ya Zanzibar ana matumaini makubwa ya kunyakua ubingwa huo.

Kocha huyo aliyasema hayo wakati alipokuwa akizungumza na gazeti hili ambapo alisema bado zipo mechi nyingi ambazo zinampa matumaini ya kushinda na kufanya vyema hatimae kutwaa kombe hilo.

“Kuwa nyuma katika ligi sio sababu itakayonifanya nisichukue ubingwa, matumaini yangu na kikosi kizima cha Malindi msimu huu kombe ni letu,”alisema.

Badru alisema anajipa matumini ya kuchukua ubingwa huo kutokana na uimara waliokuwa nao wachezai wake, katika mazoezi waliyokuwa wakiyafanya wakati ligi ilimesimama kupisha kombe lamMapinduzi.

Alieleza kwamba mechi ya kirafiki waliocheza na Azam FC inayoshiriki ligi kuu Tanzania Bara, imewasaidia wachezaji na kuwa tayari kwa kukabiliana na timu yoyote.

Alifahamisha kwamba katika mechi hiyo ya kirafiki ilimsaidia kujua kiwango cha wachezaji wake ili katika dirisha dogo aweze kusajili wanachezaji ambao watahitajika kuongezwa.

“ Mechi yetu na Azam imenisaidia sana kwa sababu nilikua naangalia kikosi changu kipo katika hali gani lakini pia mechi hiyo imenipa nafasi kuchagua wachezaji watakaonifaa wakati wa usajili wa dirisha dogo ukifika,”alisema.

Kocha huyo alieleza kwamba wachezaji wake wote muhimu katika kuhakikisha timu yao inafanya vizuri na kuchukua ubingwa wa ligi kuu.

Badru aliwaomba mashabiki na wapenzi wa timu hiyo kuendelea kuiunga mkono huku wakiwa na matumaini ya kufanya vizuri katika mechi zote zilizobakia .