NA MARYAM HASSAN

WAFANYAKAZI wa Mamlaka wa viwanja vya ndege Zanzibar wameungana na Taasisi mbalimbali za kiserikali na zisizo za kiserikali katika usafi wa mazingira kuelekea kilele cha sherehe ya miaka 57 ya Mapindyzi ya Zanzibar.

Akizungumza mara baada ya kumaliza usafi huo uliofanyika katika maeneo ya mamlaka ya viwanja vya ndege Mkurugenzi Rasilimali watu na Utawala wa Mamlaka ya Viwanja vya ndege, Muhidini Talib Abdallah, alisema, hatua hiyo ni moja wapo wa kuunga mkono kauli ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi kutaka mji wa Zanzibar kuwa safi.

Alisema, usafi huo ni moja ya mikakati ya kusheherekea Sherehe ya Mapinduzi ya Zanzibar na maeneo yote yawe safi ambapo mamlaka wameshajihika na wamejitokeza kwa wingi katika kufanya usafi usafi.

Aidha, aliwahamasisha wananchi wa Zanzibar kuendelea kudumisha utamaduni wa Wananchi wa Zanzibar kuendeleza usafi kwa kusafisha mitaa yao mbalimbali ili mazingira yawe safi.

Sambamba na hayo alisema kutokana na umuhimu wa usafi katika sehemu mbalimbali wataangalia kila mwenzi kuweza kufanya usafi katika ofisi zao, ili kuweza kuweka maeneo safi yote.

Afisa uhusiano wa mamlaka hiyo, Mulhat Yussuf Said, alisema, kufanyika usafi huo umeweza kuwaunganisha wafanyakazi wote kwani agizo hilo limeweza kuwaweka pamoja.

Sambamba na hayo, alisema kuwa usafi huo umeweza kuondoa utabaka, kwani viongozi wa ngazi mbali mbali walishiriki katika kufanya usafi bila ya kujali vyeo vyao walivyokuwa navyo.

Nao wafanyakazi wa Mamlaka ya Viwanja Vya Ndege, walisema kuwa wamefarijika kufanya usafi kwa kushirikiana katika ofisi zao, kwani imewatia moyo kuona kuwa viongozi wapo nao bega kwa bega.

Sambamba na hayo, waliuomba uongozi wa mamlaka hiyo, kufikiria kuweka siku Moja ya kila ya mwisho wa mwenzi kufanya usafi huo, ili kuweza kuyaweka maeneo yao katika hali ya usafi.