NA MADINA ISSA
WIZARA ya Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto inatarajia kuzindua mfumo wa kufanya maombi kwa njia ya mtandao kwa ajili ya kupima virusi vya Covid 19 kwa wasafiri wanaotoka na kuingia nchini.
Akizungumza na wadau wa Utalii na Wizara ya Afya, Kaimu Waziri wa Wizara hiyo, Simai Mohammed Said, alisema lengo la kufanya hivyo ni kurahisisha upatikanaji wa huduma hizo kwa wanaohitaji.
Alisema utaratibu huo pamoja na kulenga kuokoa muda, utasaidia kuondoa udanganyifu kwa kupata vyeti visivyokuwa sahihi baada ya kipimo vinavyotolewa na watendaji wasiokuwa waaminifu.
Alisema kuwa upimaji huo utawahakikishia wageni kupatiwa huduma kwa urahisi na kwa wakati ili waweze kufika nchini wakiwa na uthibitisho wa kufanyiwa vipimo vya ugonjwa huo.
Hivyo, aliwataka wadau hao kufuata utaratibu uliowekwa ili kuondosha changamoto zinazojitokeza kwa wageni na wenyeji wanaoingia au kutoka nchini.
Akizungumzia jinsi ya mfumo huo utakavyofanya kazi, Meneja Uendeshaji Kampuni ya Rahisi Solution, Abdurahman Hassan, alisema anaehitaji huduma hiyo atalazimika kufanya maombi kwa njia ya mtandao kwa kuainisha siku anayohitaji kufanyiwa vipimo na kusafiri.
Aidha alisema kuwa baada ya kukamilisha maombi, atatumiwa majibu yake kupitia simu ya mkononi na kufanya malipo kupitia benki au simu ya mkononi.
“Mfumo huu utamsaidia mtaka huduma kwani unarahisisha upatikanaji wa huduma bila ya usumbufu wa aina yoyote,” alisema.
Nao wadau wa sekta ya utalii waliiomba serikali kuangalia suala la bei ya kufanya vipimo kwa wasafiri watakaotumia mfumo huo ili kutokutofautiana kwa fedha za malipo kwa vituo binafsi na serikali.
Dk. Miraji Ukuti Ussi, kutoka Kamisheni ya Utalii Zanzibar, alisema kuwa utaratibu huo utarahisisha upatikanaji wa cheti cha kusafiria sambamba na kuondoa msongamano kwa watu wanaohitaji huduma kabla ya kuanza na safari.
“Awali tulikuwa tunashuhudia mtaka huduma anamfata mtu ila kuja hii huduma itaweza kutusaidia kwa kutuhakikishia kupata cheti kwa wakati muafaka sambamba na kupunguza gharama kwa wadau wa utalii na watalii kwa ujumla,” alisema Dk. Miraji.
Naye, Talib Jussa, alisema kuwa mfumo huo utarahisisha upatikanaji wa huduma na kupunguza msongamano wa kufika katika kituo cha kupimia virusi vya ugonjwa huo.
Hata hivyo, alisema kuwa kwa sasa wamekuwa wakipata ushirikiano mkubwa na Wizara ya Afya kwani wamekuwa wakiwapatia maelekezo yaliyokuwa mazuri na kuwarahisishia wadau wa utalii pamoja na watalii wanaoingia nchini.
Sambamba na hayo, aliipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kasi yake ya utendaji wa kufanya kazi hasa katika sekta ya Afya na Utalii ambayo itaondoa uwezekano wa maradhi mbalimbali kuingia nchini.