ADDIS ABABA, ETHIOPIA

OFISI ya Umoja wa Mataifa inayoratibu Masuala ya Kibinadamu (UNOCHA) imesema, kuvurugika kwa hatua za usimamizi na udhibiti wa maambukizi ya virusi vya Corona katika mkoa wa Tigray nchini Ethiopia kutokana na mapigano, kunaweza kuchochea maambukizi makubwa ya virusi hivyo katika jamii.

Katika ripoti yake iliyochapishwa Ofisi hiyo ilisema, vurugu hiyo iliyodumu kwa zaidi ya mwezi mmoja, pamoja na watu kukimbia makaazi yao na msongamano mkubwa wa watu katika kambi, zinahisiwa kuongeza kasi ya maambukizi ya virusi hivyo katika jamii.

Kwa mujibu wa Ofisi hiyo, hatua za udhibiti zilianza tena, ikiwemo kugawa vijarida vinavyoelekeza jinsi ya kujikinga na maambukizi ya virusi hivyo na usafi, pamoja na mavazi ya kujikinga.

Kabla ya vurugu kutokea, mpaka mwisho wa mwezi Oktoba mwaka jana, mkoa wa Tigray ulikuwa na kesi 6,610 zilizothibitishwa kuwa na maambukizi ya virusi vya Corona.