Yasherekea kwa mtindo wa kuvutia

Dk. Mwinyi kupokea maandamano

Hotuba kuitoa kupitia vyombo vya habari

NA MWANADISHI WETU

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, atakuwa mgeni rasmi kwenye hafla ya kuyapokea maandamano ya wananchi yenye lengo la kuunga mkono mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964.

Itakumbukwa kwamba tarehe kama ya leo miaka 57 iliyoyopita, wazee waliongozwa na Sheikh Abeid Amani Karume waliongoza mapinduzi na kuung’oa utawala wa kisulatani.

Sherehe, shamrashamra na maadhimisho ya mapinduzi yananyika kwa staili ya aina yake chini ya serikali mpya ya awamu ya nane iliyoingia madarakani Mwezi Novemba mwaka jana.

Dk. Mwinyi atayapokea maandamano hayo katika viwanja vya Mnazimmoja vilivyopo mjini Zanzibar, ikiwa ni kilele cha maadhimisho hayo ambapo hotuba yake ya maadhimisho inatarjiwa kutolewa kupitia vyombo vya habari.

Sherehe za mwaka huu za kuadhimisha kilele cha mapinduzi zimefanyika tofauti na miaka mingine ambapo tulizoea kuziona zikifanyika katika viwanja vya Amani kwa Unguja ama Gombani Pemba, ambapo pia hupambwa kwa gwaride.

Kabla ya kilele cha maadhimisho hayo, shamrashamra za miaka 57 ya mapinduzi zilitanguliwa na uwekaji wa mawe ya msingi na uzinduzi wa miradi ya kimaendeleo katika maeneo mbalimbali ya Unguja na Pemba.

Taarifa ambayo ilitolewa hapo awali na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais, Sera Uratibu na shughuli za Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Dk. Khalid Salum Mohamed, alisema jumla ya miradi 12 ambapo ilizinduliwa katika shamrashamra hizo.

Waziri huyo, alisema miradi hiyo ilifunguliwa na kuwekewa mawe ya msingi na viongozi wakuu wa kitaifa wakiwemo wa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano.

Aidha waziri huyo alisema kwenye kilele cha sherehe hizo kutafanyika maonesho ya amsha amsha na mapinduzi yatakayofanywa na vikosi vyote vya ulinzi na usalama vilivyopo Zanzibar pamoja na maandamano ya wananchi wa Mikoa Mitano ya Zanzibar.

Alisema maonesho ya amsha amsha yanatarajia kuanza katika viwanja vya Garagara Mtoni saa 12:00 asubuhi na kumalizia katika viwanja vya Mnazimmoja Mjini Unguja.

Alisema vikosi hivyo vitajigawa katika makundi matatu ambayo yatapita njia tatu tofauti ikiwemo ya Garagara, Maruhubi, Saateni, Ziwani Polisi, wengine ni Garagara, Maruhubi, Darajani, Ziwani Polisi na Garagara, Darajabovu Magomeni, Ziwani Polisi.

Alisema baada ya kukusanyika katika viwanja hivyo vikosi hivyo vitaondoka katika viwanja vya Ziwani Polisi na kuwasili katika viwanja vya Mnazi Mmoja kwa mapokezi rasmi mnamo saa 3:30.

Waziri huyo, aliwataka wananchi wote kuhudhuria kwa kujipanga katika barabara ambazo maonesho hayo yatapita pamoja na kushiriki katika shughuli ya mapokezi katika viwanja vya MnaziMmoja ambapo mgeni rasmi ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi na baadae atatoa salamu fupi.

Wakati sherehe hizo zikifanyika hapo jana wananchi wa Zanzibar walishuhudia mkesha wa kilele cha sherehe hizo, kwa fashi fash zilizopigwa usiku wa kuamkia leo na Jeshi la Wananchi Tanzania, (JWTZ) katika viwanja vya Maisara Mjini Unguja na Tibirinzi Chakechake Pemba.

Mambo mengine ambayo yalifanyika katika maadhimisho hayo ni pamoja na mazoezi ya kitaifa yalioanza saa 12:00 Asubuhi katika viwanja vya Mnara wa Mapinduzi Michenzani (Mapinduzi Square) kupitia Bi Ziredi, Mikunguni hadi Uwanja wa Amaani Unguja ambapo  Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi aliyaongoza.

Hapo kesho usiku, sherehe hizo zitaadhimishwa kwa kumalizia kwa fainali ya mashindano ya Kombe la Mapinduzi yalioanza Januari 5, 2021, yaliyozishirikisha timu kutoka Unguja, Pemba na Tanzania Bara, yatayofanyika Uwanja wa Amaan Mjini Unguja,