ZASPOTI

NA ABOUD MAHMOUD

NI mwaka mmoja na miezi mitano hivi sasa tangu kufariki kwa msanii nguli wa muziki wa taarab ndani na nje ya Zanzibar ambae alipata umaarufu kupitia fani hiyo na si mwengine bali ni almarhum Khadija Omar Ahmed.

Kadiri binadamu anavyokuwa mweledi wa mambo mbali mbali yenye maslahi kwake na kwa jamii inayomzunguka,kamwe hawezi kuyakinga mauti pale yanapokunjua mikono kumtwaa wakati wake ukiwa umeshafika.

Lililo muhimu kwa binadamu yoyote ni kuhakikisha matendo anayoyafanya katika uhai wake hayaachi athari mbaya kwa wenzake mara anapoondoka kwenye mgongo wa ardhi.

Malaika wa umauti ametimiza kazi yake aliyotumwa na mola wake kumuita msanii maarufu Khaija Omar Ahmed almaaruf Khadija Baramia ambae ameitikia wito huu hivi karibuni kwenye safari iliyo faradhi kwa kila kiumbe.

Miongoni mwa misiba iliyowagusa ndani ya mitima wananchi wengi wa Zanzibar,Mikoa ya Tanzania,Falme za Kiarabu na hata Bara la Ulaya na Marekani ni msiba wa msanii huyo ambae aliipeperusha vyema bendera ya Zanzibar katika fani yake hiyo.

Ni wazi maandiko ya Mwenyezi Mungu hakuna kamwe raba inayoweza kuyafuta, kwani matibabu na huduma bali mbali za kutaka kurefusha maisha yake zilichukuliwa ili kuweza kurudisha hali yake kama mwanzo lakini tayari siku na ahadi yake imefika kurudi kwa Mola wake.

Kihistoria marehemu Bi Khadija Baramia alikua msanii wa utunzi wa mashairi ya nyimbo za taaarab pamoja na uimbaji ambao fani hiyo aliitumia miaka mingi sana ambapo fani hiyo iliweza kujizoela sifa nyingi na umaarufu .

Kipaji na uweledi wa hali ya juu katika fani hiyo,ndivyo vilivyoinua jina lake hadi kuwa miongoni mwa wasanii wanaopigiwa mifano na chipukizi na wengine wanaopendelea kujifunza kupitia kwake.

Ni ukweli usiofichika kama utapita katika mitaa mbali mbali ya mjini Unguja ukitaja jina la Baramia basi ni hakika utapelekwa katika mitaa ya Kikwajuni kwani ndipo familia hiyo inapoishi tangu miaka ya zamani.

Lakini ni wengi wanafahamu kwamba marehemu alikua msanii peke yake kumbe mbali na fani ya usanii alikua na vitu vingi sana na ni mtu mmoja ambae amekua mstari wa mbele katika nyanja mbali mbali za kuitangaza vyema Zanzibar.

Baada ya kufariki kwake mwandishi wa makala hii alifika nyumbani kwa marehemu Chukwani nje kidogo ya mji wa Zanzibar na kukutana na mdogo wake marehemu ambae nae hivi sasa pia ameshatangulia mbele ya haki, Marehem Bi Salma Baramia na kumuelezea vitu mbali mbali alivovifanya marehemu wakati wa uhai wake .

Ingawa bado yupo na majozi ya kuondokewa na dada yake lakini tulikwena hatua kwa hatua mwanzo hadi mwsiho wa mazungumzo yetu.

Marehemu Khadija Baramia alizaliwa mwaka 1947 katika mtaa wa Vikokotoni akiwa ni mtoto wa tatu katika familia ya watoto nane sita wanaume na wawili wanawake ambapo elimu yake aliianzia katika skuli ya Kikwajuni maarufu kwa Mselem na kumalizia elimu ya sekondari katika skuli ya Benbella.

Mara baada ya kumaliza masomo yake marehemu aliajiriwa katika Wizara ya Kilimo akiwa katika nafasi ya Karani ambapo alifanya kazi hiyo kwa miaka mingi mpaka kustaafu kwake.

“Marehemu alipomaliza masomo yake alikua muajiriwa wa Serikali katika Wizara ya Kilimo ambapo alifanya kazi kwa muda mrefu kwahiyo sio kama mara kumaliza skuli alikua msanii,”alisema Salma.

Mara baada ya kustaafu kazi hiyo Marehemu Khadija Baramia alijiunga katika mchezo wa netiboli akiwa mwamuzi wa mchezo huo ambapo alisema nafasi yake hiyo ya uwamuzi iliweza kumfanya ashiriki katika mashindano mbali mbali ya kitaifa na kimataifa.

“Marehemu alikuwa mwanamichezo wa mchezo wa netiboli na alikua mwamuzi katika mchezo huo ambapo aliweza kushiriki katika mashindano mbali mbali ikiwemo yale ya Afrika Mashariki na Kati, mashindano ya Chalenji na hata katika ligi za taifa za Zanzibar na Tanzania kwa ujumla,”alisema.

“Nakumbuka akiwa mwanamichezo aliwahi kushiriki katika mashindano ya Comon Wealth yaliofanyika nchini Urusi akiwa ni miongoni mwa viongozi waliofatana na wachezaji wa mpira wa netiboli na wananyanyua vitu vizito,”aliongezea.

Mbali na fani ya michezo marehemu Khadija Bramia alikua miongoni mwa waasisi wa Umoja wa Wanawake Tanzania Zanzibar (UWT) kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM)akiwa na akina mama wengine akiwa Bi Asha Simba.

Kuhusu mambo ya sanaa Marehemu alikua msanii kipindi kirefu sana na fani hiyo aliianza akiwa bado hajaolewa na alianza katika maswala ya utungaji wa nyimbo ambapo alianza na kutunga nyimbo katika kikundi cha Nadi Ikhwan Safaa.

“Fani ya usanii marehemu alianza tangu akiwa mwanamwari mana alitunga nyimbo kadhaa ikiwemo nyimbo ‘Nimeridhi pendo langu’ na nyengine nyingi lakini fani hiyo ndani ya damu ipo mana mama yetu alikua msanii na kaka yetu pia alikua msanii,”alisema.

Kwa hakika mpenzi wa msomaji kama utazikumbuka nyimbo za taarab zinazojulikana kwa jina la ‘Mcheza ngoma si yake na nyengine Paka shume’ pamoja na mashairi mengi yaliokua yakiandikwa kwenye gazeti la Zanzibar Leo utunzi wa kaka wa marehem Khadija baramia ambae nae pia ameshafika mbele yake marehemu Ali Omar Baramia.

katika miaka ya nyuma taarab ilikua ikiimbwa na wanawake watupu ambapo ilikua ikiimbwa kama burudani kwenye maharusi na bila ya kutumia spika na huimba wenyewe ndani tu, na vikundi hivyo vya Taarab vilikua vingi ikiwemo Nour L- Uyoun,Sahib L-Ari, Royal Air Force na Nevi ambavyo vyote vilikua vya wanawake.

“Nour L-Oyoun kilikua kikundi cha nyumbani ambapo marehemu mama yetu ndio alikua kiongozi wa kikundi hicho na walikua wakiimba wenyewe kwa wenyewe, na nyimbo zilikua zinaimbwa na watu wengi tofauti na sasa nyimbo moja inaimbwa na mtu mmoja,”.

Marehem Salma alisema mwaka 1977 kulikua na harusi ya mtu aliemtaja kwa jina la Arafata Abdulqadir maarufu Arafata Mbude hivi sasa ni marehemu, aliimba nyimbo kipande kimoja na hapo ndipo watu wengi waliona kipaji chake na watu wengi walifurahi hususan marehem mama ake kwani kipindi kirefu baada ya kufiwa na mume wake marehemu alikua ni mwenye majonzi.

Kutokana na sauti yake kuwa ndogo aliwashuari wazee wa kikundi hicho kuweka spika na kwa mara ya kwanza katika harusi hiyo hiyo ya marehemu Arafata Mbude kuliwekwa spika na viti na watu wengi walianza kuona kipaji chake na akaendelea na fani hiyo.

Kutokana na kukinyanyua kikundi hicho cha Nour L Uyoun hapo hapo vikundi vyote vya wanawake navyo vilishajiika na kuamka zaidi ingawa kikundi hicho kilikua zaidi kutokana na kilikua kina mtunzi wa nyimbo na zilikua nzuri.

Marehemu alitunga nyimbo nyingi sana kama vile Uwa, Bustani, Kisima, Hata Haikua, Siku ya masiku,Mapenzi yamenisibu,Mapenzi yako matabu, Nibras,Wakusifiwa ni nani na nyengine nyingi ambazo mpaka hivi sasa bado zinapendwa nyimbo hizo.

Kipaji cha marehemu Khadija Baramia kilionekana kuvutia watu wengi sana kwani wakati akiinuka na kuanza kuimba watu wengi sana huinuka na kufurahia uimbaji wake jinsi ya sauti yake ya kumtoa nyoka pangoni na mashairi yaliyopangika .

Moja ya beti ya nyimbo ya mapenzi yako matamu ni kama ifuatavyo
“Yarabi atudumishe, Mapenzi yetu yadumu
Mapenzi tuyazidishe,Yawachome wanadamu
Furaha kwetu zisishe,Kwa nguvu zake karibu

Mapenzi yako matamu yasalam yasalam
Mapenzi yako timamu yasalam yasalam
Kukicha yazidi hamu, Kukicha yazidi utamu.

Mara ya kwanza kwa msanii huyo kupanda katika jukwaa na kuimba mbele ya viongozi mbali mbali wa kitaifa akiwemo Rais wa Kwanza wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzanzia,Hayati Mwalimu Julius Nyerere katika shere ya kitaifa iliyofanyika katika mji mkuu wa Tanzania Mkoani Dodoma.

Hii yote inajidhihirisha kwamba marehemu Khadija Baramia alikua na ubunifu wa hali ya juu katika fani hiyo ya sanaa kwani mbali na uimbaji na utungaji lakini pia aliweza kuwakusanya wanawake wa vikundi vyote vya taarab vya wanawake na kuanzisha kikundi cha taifa cha wanawake ambacho ndicho kilichoenda kutumbuiza Dodoma.

Kauli ya Salma inasema kwamba marehemu hakuwa mwanachama rasmin wa kikundi cha Nadi Ikhwan Safaa bali alikua muimbaji mualikwa na alikua akipeleka mashairi yake na baadae kutiwa muziki na kuimbwa na wasanii mbali mbali ikiwemo Nimeridhi Pendo langu,Halitujii nyoyoni jambo la kufarakana.

Lakini mbali na maswala ya ya sanaa marehemu ni miongoni mwa waasisi wa gazeti la Sauti ya Siti ambalo lilikua chini ya Uongozi wa Chama cha Wandishi wa Habari Wanawake Tanzania(TAMWA).

Kwa upande wa familia Salma alisema marehemu alikua nguzo ya familia katika nyanja mbali mbali kwani alikua akiiongoza familia na kuiweka pamoja katika kutatua matatizo na hata wakati wa shughuli wanakua kitu kimoja.

“Marehemu hakua dada kwetu wala hakua mama peke yake bali alikua ni kiongozi na nguzo ya familia ambayo bado tunamuhitaji mana katika sekta yeye kwetu alikua mstari wa mbele kusaidia kwa hali na mali mpaka jambo lifanyike lakini mipango ya Mungu haina makosa haujua Mungu ametupangia nini au atatupa nani wa kuingoza familia lililobaki ni kumuombea Allah ampe pepo ya firdaus na sisi Allah atupe subra,”alisema.

Mwandishi wa makala hii hakuishia kwa familia ya marehemu aliweza kufanya mahojiano na watu mbali mbali wakiwemo wasanii wa zamani, wasanii wa sasa hivi, jirani zake wa mitaa ya Kikwajuni na Kisimamajongoo pamoja na watu wa karibu na marehemu.

Kwa ukweli kila mtu aliezungumza na mwandishi wa makala hii hakuacha kumsifia marehemu kutoka na vitu mbali mbali na kipaji alichojaaliwa na Mwenyezi Mungu ikiwemo ukaribu, msaada na ihsan pamoja na kuishi na watu kwa uzuri.

Saleh Mussa Maisara ni miongoni mwa wasanii ambao wamekua karibu sana na marehemu bi Khadija Baramia nae hakusita kumuelezea namnan anavyomfahamu marehemu katika fani ya sanaa na hata nje ya maswala ya sanaa.

“Marehemu Bi Khadija Baramia alikua mama angu na mama angu sio kama kanizaa lakini ni mama angu alienilea tangu nikiwa mdogo nilikua nipo nyumbani kwake na sababu ya mimi kujiunga katika fani hii ya usanii wa kupiga muziki yeye ndie alienishawishi mpaka nikajikuta nimetumbukia kwenye fani hii,”alisema.

“Nilipokua mdogo nikiwa nyumbani kwake na yeye akiwa Mkurugenzi wa kikundi cha Nour L Uyoun na mama ake marehemu bi Mwanafatuma akiwa kiongozi mkuu wa kikundi hicho nilikua nasikiliza namna ya kupiga vinanda kitoka kwa mpigaji wao mkuu alikua anaitwa Kombo ndipo na mimi nikajifundisha na hatimae nikawa najua kutumia ala za muziki,”aliongezea.

Saleh alisema kikundi chake cha mwanzo yeye kupiga taarab kilikua na Nour L Uyoun na nyimbo nyingi sana alizoimba marehemu yeye ndio aliekuwa akimpigia kinanda baada ya marehemu mwenyewe kuzitunga nyimbo hizo.

“Nimeondokewa na hili ni pigo kwangu kwani marehemu alikua mama angu wa kila kitu sio kwenye maswala ya sanaa tu lakini hata katika mambo mengine yeye ndie alikua mstari wa mbele kunisaidia wakati ninapokutwa na matatizo yeye pia ndio alionionesha njia ya kufanya kazi hii na kujikwamua kimaisha,”alisema huku akibubujikwa na machozi.

Saleh alifafanua kuwa marehemu aliweza kutunga na kuimba nyimbo nyingi ndani ya kikundi hicho cha wanawake ambapo alizitaja baadhi ya nyimbo zake ni ni pamoja na Uwa, Bustani, Siku ya masiku,Nampenda mpenzi wangu katu simwachi,Kisima,na nyengine nyingi.

moja ya beti ya nyimbo uwa ni kama ifuatavyo.
Sikusudii lawama, Kuwalaumu wenzangu
wanaonisema sema,Mimi na mpenzi wangu
Nimezama nnasema,Mesabili pendo langu
Kuwa nae ni lazima,Ni uwa la Moyo wangu

Wacheni kulia wivu, Tunopendana ni sie
Bure wenu uchukivu, Mtajiudhi wenyewe.

Makala hii ilizungumza na msanii mahiri wa kike nchini bibi Maryam Hamdan na kumuelezea jinsi anavomfahamu marehemu na kusema kwamba ameanza kumjua marehem wakati ameshakua msanii na kiongozi
wa kikundi cha wanawake cha Nour L Uyoun.

“Marehemu nimemfahamu wakati kishakua msanii mimi mara ya mwanzo nilimuona katika taarab ya kikundi chake na nikasema mashaallah msanii ana sauti nzuri sana hapo ndipo nilipoanza kumfahamu na ndipo tukawa tunafahamiana kisanii mana hata nilipoanzisha kikundi cha Tausi alikuja akazungumza na wasanii wangu kuwaeleza umuhimu wa fani hii na pia kuwa wastahamilivu na kujiendeleza zaidi kisanii,”alisema.

Nae msanii Profesa Mohammed Ilyas alisema kwamba kumfahamu kwake msanii huyo kumetokana na utunzi wa nyimbo na uimbaji wake katika kikundi cha Nadi Ikhwan Safaa ambapo alikua akialikwa na kwenda kuimbia hapo.

Alisema kwamba nyimbo nyingi marehemu alikua akitunga na yeye alikua anamtilia mashairi na kuwapa wasanii wengine wakiimba na hata nyengine akiimba yeye mwenyewe

“Khadija kwangu ni ndugu na pia ni dada angu kwa sababu tulikua tunaheshimiana sana na pia tulikua tunasaidia katika maswala ya usanii yeye alikua anatunga nyimbo ananiletea mimi natiwa muziki na pia alikua ni mtu hodari aliimarisha vikundi vya wanawake,”alisema.

Ilyas alisema moja ya nyimbo aliyotunga marehemu na muziki alitia yeye ambapo alisema nyimbo hiyo ilighaniwa na Al anisa Aziza Abdullah inajulikana kwa jina la ‘Niibe’

Mashairi ya nyimbo hiyo yanasema kama ifuatavyo
“Niko radhi kuibwa, Madhali mwizi ni wewe
Kwenye hatari kutiwa,Nimekubali mwenyewe
Niibe nipate tuwa, Kinipungue kiwewe”.

Kwa upande wa majirani nilifika kwa mama au mzee miongoni mwa wazee wa mtaa wa Kisimamajongoo ambae anamfahamu vizuri marehemu aliejitambulisha kwa jina la Bi Mwannuru nae alisema kwamba marehemu anamjua tangu akiwa mdogo mpaka amekua mtu mzima na kuhamia hapo .

Alimsifia marehemu kwa kusema kwamba hakua mtu tabu hakua mtu wa kujinata na kila mmoja alisema alikua ndugu kwake na alifanikiwa kuwafaa au kuwasaidia wengi mtaani hapo.

“Khadija ndugu yangu mimi namjua tangu akiwa mdogo mpaka amekua mtu mzima amehamia hapa mimi nipo nimempokea na alikua ana heshimu kama dada ake lakini pia sio mimi tu hapa mtaani watu wote yeye wake hapa ana mama ana dada ana ndugu ana watoto na wajukuu kwa hapa mtaani yeye wote kwake ni sawa na amesaidia vijana wengi hapa mtaani kwetu Alhamdulilah na sio kama ndo anasaidia kuwa ana uwezo anasaidia kuwa hataki kuona vijana wakikaa tu bila kujishughulisha au wakihangaika,”alifafanua.

Marehemu Khadija Baramia ameugua kwa muda mfupi na alifariki Septemba 23 mwaka 2019 Royal Hospital nchini Muscat Oman ambapo alikuepo huko akipata matibabu hadi kifo chake kumkuta na usiku wa kuamkia siku Ijumaa maiti yake ilipokelewa katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Abeid Aman Karume uliopo Kisauni Zanzibar.

Shughuli za mazishi za marehemu zilifanyika hapo hapo nyumbani kwao Kikwajunu karibu na msikiti Duara na baadae kupelekwa msikiti wa Weles kwa ajili ya ibada ya kuswalia na mwisho kupelekwa kwenye nyumba yake ya milele katika makaburi ya Mwanakwerekwe.

Mwenyezi Mungu amsameh makosa yake na kumuondoshoa adhabu ya kaburi Amiin.