WASHINGTON, MAREKANI

MAREKANI imelikataa ombi la Umoja wa Mataifa la kubadilisha uamuzi wake wa kuwatangaza waasi wa Houthi nchini Yemen, kuwa kundi la kigaidi.

Umoja wa Mataifa na maofisa wa ngazi ya juu wa mashirika ya umoja huo waliitaka Marekani kubadili uamuzi wake huo kwa lengo la kuzuia njaa na vifo kwenye taifa hilo lililoharibiwa kwa vita.

Naibu Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, Richard Mills aliliambia Baraza la Usalama la umoja huo kwamba wanaamini hatua hiyo ni sahihi kupeleka ishara kwamba wanataka mchakato wa kisiasa kusonga mbele.

Balozi Mills alisema amesikiliza tahadhari zilizotolewa kuhusu athari ya kibinaadamu kutokana na kuwatangaza waasi wa Houthi kuwa kundi la kigaidi.

Alisema Marekani itachukua hatua kupunguza athari za upelekaji wa misaada na uagizaji wa bidhaa za kibiashara.