MICHUANO ya Kombe la Mapinduzi inaendelea kutimua vumbi kwenye uwanja wa Amaan ambapo klabu tisa zinashiriki michuano hiyo ya 14 tokea kuasisiwa kwake mwaka 2007.

Miamba hiyo ni pamoja na mabingwa watetezi, Mtibwa Sugar, Simba, Yanga, Namungo na Azam kwa upande wa Tanzania Bara huku Jamhuri, Chipukizi, Malindi na Mlandege kwa Zanzibar.

Tunachukuwa nafasi hii kuendelea kuzitakia ushiriki mwema klabu zote tukiamini itakuwa ni michuano itakayokuwa na ushindani mkubwa na kuleta msisimko kwa mashabiki watakaokuwa wakiishuhudia kwa karibu wiki mbili.

Tunaamini maandalizi yote yamekwenda vizuri katika kuzifanya timu shiriki zijihisi kweli zipo kwenye mashindano bora na yenye kushabihiana na hadhi ya klabu zao badala ya kuonekana kama mashindano ya mitaani.

Kama tunavyofahamu, michuano ya Kombe la Mapinduzi ni michuano inayoendeshwa kwa murtada wa sherehe zenyewe za Mapinduzi ya Zanzibar ya Mwaka 1964 ambayo yalimkomboa Mzanzibari kutoka utawala wa kikoloni na usultani.

Hivyo basi haitapendeza kuiona michuano hiyo kama ndondo za mitaani kwa kukosa mpangilio na usimamizi bora au malalamiko ya mara kwa mara kutoka kwa timu shiriki juu ya ushiriki mzima wa michuano hiyo.

Hilo ni moja, lakini, jambo jengine tunalolishauri hasa kwa timu zetu za Zanzibar kuifanya michuano hiyo kama darasa upande wao kwa kujifunza aina ya ushindani unaohitajika huku ikizingatiwa kuwa timu zetu zimekuwa na matokeo mabaya wakati zinaposhikiriki michuano ya kimataifa.

Ni ukweli usiopingika kuwa michuano imekuwa ikivuta hisia za mashabiki wengi kutokana na aina ya ushindani unaoneshwa na timu zishiriki hasa zile zinazotoka nje ya Zanzibar.

Hivyo kwa kuitumia michuano hiyo, klabu zetu zitakuwa na mengi ya kujifunza katika kupata matokeo mazuri ikizingatiwa miongoni mwa wawakilishi wetu hao wanacheza Ligi Kuu ya Zanzibar ambayo ndiyo inayotoa wawakilishi wa kimataifa.

Tunaamini baada ya kujitathmini huko, watajipanga na kuzifanyia kazi kasoro watakazoziona na kujipanga kiushindani zaidi kwa mashindano yatakayokuwa mbele yao.Kutokana na hali, tungelipenda kuwashauri waandaji kwamba upo umuhimu wa kuyatazama kwa jicho la tatu michuano hiyo kwani kuwepo kwake kumebeba taswira kubwa ya Mapinduzi,lakini, pia tunaweza kuyatazama kama sehemu bora ya kujitathmini kwa wawakilishi wetu.Kila la heri Kombe la Mapinduzi 2021.