NA MWAJUMA JUMA
MASOUD Tawakal Khairalla ni mwanaridha mkongwe wa Zanzibar ambaye anaendelea kushikilia rekodi ya Tanzania ya kuruka juu ya mita 2:00 ambayo aliiweka mwaka 1978 kwenye mashindano ya Majeshi yaliofanyika Tanzania Bara.
Awali rekodi ya taifa ilikuwa inashikiliwa na Layuni Sumuni Mmasai.

MASOUD Tawakal

Khairalla alizaliwa tarehe 5 Septemba mwaka 1954 na kuanza elimu yake ya msingi mwaka 1960 katika Skuli ya Bububu wilaya ya Magharibi ‘A’ na kumalizia masomo yake katika Skuli ya Dole mwaka 1968.

Kipaji chake katika mchezo wa riadha kilianza kung’ara tokea akiwa skuli ambapo mwaka 1968 alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa kuruka juu.
Mnamo mwaka 1970 alijiunga na Umoja wa Vijana wa ASP na akawa anacheza timu ya mpira wa miguu katika nafasi ya mlinda mlango.

Mnamo mwaka 1971, aliajiriwa rasmi na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), kupitia mchezo huo, ajira ambayo aliitumikia mpaka kufikia muda wa kustaafu.
Khairalla hakuwa mwanariadha pekee bali pia alikuwa mchezaji wa soka, mpira wa kikapu na mpira wa mikono ambayo ilimfikisha katika mashindano ya Afrika Mashariki mwaka 1978.

Mwaka 1976, alipata nafasi ya kuingia timu ya taifa kupitia mchezo wa kuruka juu na chini na kuruka kwa upondo na kushiriki michuano ya majeshi Zanzibar.
Anasema, mnamo mwaka 1977 alichaguliwa kwenye timu ya vijana ya Tanzania ambayo ilishiriki michuano ya dunia nchini Ugiriki na alifanikiwa kushika nafasi ya tano kwa mchezo wa kuruka juu.

Anasema, mnamo mwaka 1976, walipata zawadi akiwa yeye na mchezaji mwenzake, Salum Hassan Mzee ambaye aliruka vihunzi na mwaka 1978 alisafiri na timu ya taifa ya Zanzibar kwenda Mombasa kwenye mashindano ya Afrika Mashariki na Kati kwa mchezo wa kuruka juu na kuruka na upondo na kupata nafasi ya tatu.

Aliwataja wachezaji aliokuwa nao katika kikosi hicho ni pamoja na Salum Hassan, Suleiman Ame Nyambui, marehemu Yakuti Juma, Hassan Juma Juma, marehemu Safia Maneno, Rahima Bakari, Mohammed Dahoma, Abuu Amour, Mbarouk Mohammed, Ahmed Yussuf na walichukuwa nafasi ya pili kwa ujumla.

Anasema, mnamo mwaka 1978 walikwenda nchini Somalia katika mashindano ya Ujirani Mwema ambapo walikuwa wachezaji wanane akiwemo Suleiman Ame Nyambui, Yussuf na Zainab Ali na huko alipata nafasi ya tatu kwa kuruka juu.

Aidha, anasema, mwaka 1987 walikwenda nchini Canada katika mashindano ya Jumuiya ya Madola ambapo timu hiyo ilikuwa na wachezaji saba, akiwemo Gidamis Shahanga, Suleiman Nyambui, Ndia Mandoi, Filbert Bayi na walitokea washindi wa wanane wa ujumla.

Anasema, mnamo mwaka 1982 alikwenda nchin Misri kushiriki mashindano ya Afrika na kupata ushindi wa wanne na timu pia ilitokea nafasi ya nne.
Mwaka 1984, walishiriki tena mashindano hayo nchini Misri na kutokea mshindi wa tatu, lakini, hakufanikisha kutokana na ufuatiliaji wa viongozi wake kuwa mdogo.
Alisema, nafasi hiyo aliikosa ingawa ilikuwa haki yake kwani kutokana na kanuni ya mashindano kulitokea mchezaji mmoja.

Tawakal hakuishia hapo kimichezo pekee, aliamua kujifundisha ualimu mnamo mwaka 1990 huku akiwa mchezaji na mnamo mwaka 1999 aliacha rasmi kuwa mchezaji baada ya kuumia kidole pamoja na jicho lake la upande wa kulia.
Anasema haikuwa dhamira yake kuacha kucheza kimya kimya kwani alipanga kuaga hadharani, lakini, baada ya kutokea hayo ilimbidi asifanye chochote na kuamua kuacha kimya kimya.

Anasema, kitu kikubwa ambacho anajivunia mpaka sasa ni kuwa pamoja hakusoma kwa kiwango cha juu cha elimu, lakini, kupitia michezo amebahatika kutembelea sehemu mbali mbali ndani na nje ya nchi.

“Hapa nilipo ninacho cha kuwahadithia wajukuu wangu namna michezo ilivyonipaisha na kusafiri mara kwa mara nje ya nchi”, alisema.

Anasema mnamo mwaka 2002 alipata nafasi ya kwenda nchini Uganda akiwa kocha wa timu ya taifa ya Zanzibar na kutoka na ushindi wa pili.
Aidha, anasema, hakusomea ukocha wa riadha tu, bali ni kwa michezo yote ikiwemo hata michezo ya watu wenye ulemavu ambapo mwaka 20006 alipewa timu ya taifa ya watu wenye ulemavu ya Tanzania kwenda nchini Australia kushiriki michuano ya Jumuiya ya Madola.

Anasema, katika mashindano hayo timu hiyo haikufanya vizuri na wachezaji walifungwa, lakini, licha ya kufungwa hawakuvunjika moyo na walishiriki mpaka mwisho.Anasema mwaka 2024 alipewa timu ya Taifa ya vijana ya Zanzibar kushiriki michuano ya Afrika Mashariki yaliyofanyika jijini Dar es Salaam na Zanzibar ikashika nafasi ya kwanza.

Anasema katika mashindano hayo alipata faida moja kubwa kwa kuibua mchezaji mpya wa mbio fupi katika ukanda huo wa Afrika Mashariki na Kati, Khamis Gulam ambapo nchi zilizoshiriki ni Kenya, Uganda, Ethiopia, Sudan, Zanzibar na wenyeji Tanzania Bara.

Gulamu alikimbia mbio za mita 100 na 200 na alitokea wa kwanza .Anasema, mwanariadha alipata fursa ya kufanya majaribio nchini Kenya mjini Dolet ili akifanikiwa aende katika mashindano ya dunia, lakini, hakufikia kiwango kutokana na matatizo yao ambayo hakuyaweka wazi.

Hata hivyo anaendelea kusema kuwa licha ya kuwa hakufanikiwa huko lakini mnamo mwaka 2016 mchezaji huyo alikwenda nje kwa majaribio pia.

Tawakal anasema katika safari yake ya michezo ndani ya ualimu mnamo maka 2019, alichaguliwa kuwa kocha wa timu ya walemamu wa viziwi kwenda kushiriki michuano ya Afrika nchini Kenya na Zanzibar walipata nafasi ya sita kati ya timu tisa zilizokuwa zikishiriki michuano hiyo.

Alizitaja timu ambazo zilishiriki michuano hiyo ni Algeria, Kenya, Uganda, Zanzibar na Misri ambayo ndio walioshika nafasi ya kwanza na wenyeji Kenya wakapata nafasi ya pili. “Nashukuru nimecheza na kwenye uongozi pia, licha ya kuwa kocha pia niliwahi kuwa Makamo Mwenyekiti wa Chama cha Riadha Zanzibar (ZAAA) kwa kipindi cha miaka mitano na niliongoza kwa mafanikio”, alisema.

MAFANIKIO YAKE KWA UJUMLA

Anasema kuwa katika uhai wake hakutegemea kabisa kusafiri nje ya nchi, lakini, kupitia michezo ameweza kufasafiri mpaka Australia na nchi nyengine nyingi za Afrika Mashariki na Kati.

Mafanikio mengine ambayo hatoyasahau pia ni pamoja na kupata ajira, kupata umaarufu kwa vile huwezi kuzungumza riadha pasipo na yeye kumtaja, kwa sababu mpaka leo yupo katika kitabu cha kumbukumbu cha kutovunja rekodi yake ya kuruka mita 2:00.

Kwa upamde wa changamoto anasema kuwa hakubahatika kukutana na changamoto kubwa isipokuwa changamoto ambazo alikutana nazo zilikuwa ni za kawaida tu.
Tawakal ambaye hadi sasa anaendelea na michezo akifundisha timu ya riadha ya Chemchem ya Bububuameoa, alizaa watoto 13 ambapo wawili walifariki na sasa hivi wamebakia 11, kati ya watoto hao tisa wanawake na wawili wanaume.

Aidha katika watoto wake hao mmoja wa kiume, Sleyum Masoud Tawakal amerithi mchezo wa baba yake anachezea klabu cha Mafunzo na mmoja wa kike Ruwaida Masoud Tawakal alikuwa akishiriki mpira wa kikapu katika michezo ya UMISETA.
Kwa upande wake, Tawakal walizaliwa watoto 12 wakiwemo wanawake wanne na wanaume wanane.