KABUL,AFGHANISTAN

MAZUNGUMZO ya amani kati ya serikali ya Afghanistan na kundi la Taliban yanatarajiwa kuanza tena leo huko Qatar,huku kukiwa na hofu ya kuongezeka kwa mashambulizi.

Majadiliano ya miezi kadhaa kati ya pande hizo mbili yalipiga hatua kidogo, ingawa pande zote zilikubaliana kuhusu ajenda za kujadiliwa katika awamu mpya ya mazungumzo.

Wapatanishi wa serikali ya Afghanistan watashinikiza makubaliano ya kudumu ya kusitisha mapigano na kuulinda mfumo uliopo wa utawala tangu kuondolewa kwa Taliban mwaka 2001.

Wakati huo huo,ripoti iliyotolewa na gazeti la The New York Times ilieleza kuwa zaidi ya raia 130 waliuawa mwaka uliopita nchini Afghanistan.

Licha ya kutokuwepo kwa takwimu rasmi,gazeti hilo limeorodhesha mauaji 136 ya raia na askari wa usalama 168 kwa mwaka 2020,mmoja kati ya miaka mibaya kabisa kushuhudiwa katika historia ya hivi karibuni ya Afghanistan.