NA SAIDA ISSA, DODOMA

MBUNGE wa Gando kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Salim Mussa Salim, amekerwa na suala la ajira Nchini kupewa kipaumbele wageni toka nje ya Nchi huku wazawa wenye sifa  wakiachwa na hivyo kuwataka Wabunge kusimamia na kutetea suala la utaifa.

Mbunge huyo alitoa kauli hiyo Jijini Dodoma wakati akizungumza na Gazeti hili katika mahojiano maalum.

Alisema kuwa suala la utaifa ni muhimu endapo wabunge watasimamia  katika  utoaji ajira liangaliwe kwa wazawa wenye sifa, ili kutimiza adhma ya Rais ya kujitegemea.

“Haiwezekani kazi ambayo anatakiwa kuifanya mtanzania wa kawaida lakini imekuwa ni jambo la ajabu kazi hiyo anapewa mgeni sio kwamba tunawabagua wageni bali ifike wakati wazawa wawepo,”alisema Salim.

“Suala hili ningependa liundiwe sheria kwamba ajira yeyote ambayo mzawa ana uwezo lazima apewe kipaumbele sio mgeni,”alieleza mbunge huyo.

Aidha, akizungumzia kuhusu suala la kodi mbili kwa Serikali mbili za Zanzibar na Bara, ambalo alisema limekuwa ni kero kutokana na ukiritimba uliopo licha ya kodi hiyo kwa Zanzibar kuwa na punguzo kubwa.

Katika hatua nyingine alilaumu Mamlaka ya mapato nchini TRA  kujifanya kama polisi jambo ambalo limekuwa likipelekea watu kuogopa kushindwa kufanya nao makubaliano.

“TRA jukumu lao ni kuwa rafiki na wananchi, lakini kumekuwa na kadhia kubwa pale bandarini najua namna wananchi wanavyoteseka  mtu kutozwa  kodi mara mbili kwa anayetoka Zanzibar akifika bara na gari anapaswa kulipia tena ushuru,”alisema Mbunge huyo.