NA LAYLAT KHALFAN

MWAKILISHI wa jimbo la Tumbatu, Haji Omar Kheir, amesema atashirikiana na viongozi wa jimbo hilo kuhakikisha maendeleo jimboni humo yanaimarika kwa kiwango cha juu.

Mwakilishi huyo aliyasema hayo Mkokotoni hivi karibuni, katika mkutano wa shukran kwa wananchi wa jimbo hilo kwa kuwachagua kwa ushindi wa kishindo pamoja na kusikiliza changamoto zao zinazowakabili.

Alisema miongoni mwa jitihada hizo ni kuhakikisha wanaimarisha miundombinu mbalimbali ikiwemo, barabara za ndani, vituo vya afya, elimu, vianzio vya maji ili wakaazi wa mkokotoni waweze kufaidika na huduma ya maji safi na salama.

“Hili tatizo la maji tunalijua na ni la muda mrefu, kweli mnateseka lakini hivi karibuni tutahakikisha mnapata huduma hii bila ya usumbufu,” alisema.

Mwakilishi huyo alieleza kuwa hivi sasa kijiji hicho kina ongezeko kubwa la watu, hivyo watafanya juhudi ili kuhakikisha wakaazi wa eneo hilo wanapatiwa huduma zinazostahiki bila ya usumbufu.

“Umeme ni muhimu kwa sababu unaimarisha uchumi wa mtu mmoja mmoja lakini kwanza tunaanza na maji ambayo ndio mkombozi wa kila mtu katika maisha ya binadamu,” alisema Mwakilishi huyo.

Akizungumzia kuhusu vijana, alisema wapo vijana ambao wenye elimu lakini hawana ajira, hivyo wasikate tamaa juu ya utafutaji kwani suala hilo ni la kidunia na kupelekea wengine kukosa kazi serikalini.

Naye Mbunge wa jimbo hilo, Juma Othman Hija, alisema chama cha Mapinduzi kimepata ushindi wa kihistoria hivyo hawana budi kurejesha shukran zao za dhati kwa wananchi hao.

Alisema maendeleo kamwe hayapatikani kama kutakuwa hakuna amani, umoja na uwajibikaji kwani watu wengi wanaona kuwajibika ni wafanyakazi wa serikali pekee bali watu wote wanahitaji ushirikiano ili maendeleo yaweze kupatikana kwa haraka.

Baadhi ya wananchi waliotakiwa kutoa changamoto zao, walisema eneo lao linakabiliwa na tatizo la muda mrefu la maji na kupelekea kunywa maji yasiyo salama yanayowasababishia madhara kiafya.

Kuhusu suala la umeme, walisema bado limekuwa ni kikwanzo kikubwa kwao kiasi ambacho wanashindwa kuendesha shughuli zao za kujipatia kipato.

Tunaomba tujengewe skuli hapa Mkokotoni kwani iliyopo ni ndogo na watoto wetu wanakaa chini na kushindwa kushughulikia vyema masomo yao”, alisema Makame Juma Sheha, mkaazi wa shehia ya Mkokotoni.