CAIRO, Misri
MKONGWE wa soka wa Al Ahly, Emad Meteb, ametoa ushauri kwa wachezaji wa sasa kabla ya kampeni yao ya Kombe la Dunia la Klabu, inayotarajiwa kuanza mwezi Februari.
Michuano hiyo itafanyika kati ya Februari 1 na Februari 11 huko Qatar na viwanja viwili vimewekwa kuandaa michezo hiyo, Ahmad Bin Ali na viwanja vya Education City.


Mechi ya ufunguzi ilitakiwa kuwa kati ya mabingwa wa Qatar, Al Duhail na Auckland City ya New Zealand. Lakini, Auckland ilitangaza kujiondoa kwenye michuano hiyo kwa sababu ya ‘corona’.
Kwa hali hiyo, raundi ya kwanza haitafanyika tena na Al Duhail itaanza michuano hiyo kutoka raundi ya pili ambapo wamepangwa dhidi ya mabingwa wa Afrika, Al Ahly.
Emad Meteb, ambaye alicheza mara nne akiwa na ‘mashetani wekundu’ hao kwenye mechi tano za awali kwenye Kombe la Dunia la Klabu, alisema, ili wachezaji waweze kupata kitu maalum, lazima wachukue mchezo mmoja kwa wakati mmoja.


“Usifikirie kushiriki Kombe la Dunia la Klabu sasa,” Meteb, alisema.
“Nilishiriki Kombe la Dunia la Klabu mara nne, na tulifanya makosa. Tuliposema kwamba tutashinda mashindano hayo, tulipata nafasi ya sita.
“Wakati hatukufikiria juu ya hilo na kuondoa shinikizo kutoka kwetu, tulipata nafasi ya tatu.
“Manuel Jose, kocha wa kihistoria wa Al Ahly, alituambia michuano hii ni heshima kwako kwa kushinda Ligi ya Mabingwa ya CAF. Furahia hafla kubwa zaidi na fikiria kila mechi kivyake.


“Ninasema kwa wachezaji, msifikirie kukutana na Al Duhail au Bayern Munich, fikiria juu ya kukutana na Pyramids, kisha furahia Kombe la Dunia, na tuone ni wapi utafika.
“Shughulikia kila mechi kulingana na mazingira yake, na tuone ni nini kitatokea”.
Emad Meteb ndiye mchezaji wa kwanza wa Misri na Al Ahly kufunga kwenye Kombe la Dunia la Klabu, wakati alipocheka na nyavu dhidi ya Sydney FC kwenye Kombe la Dunia la Klabu la 2005.


Alicheka tena nyavu katika mechi ya mwisho kwenye michuano hiyo dhidi ya CF Monterrey, na kwa jumla, alifunga mara mbili katika michezo tisa
Al Ahly bado wamebakiza mchezo mmoja kwenye Ligi Kuu ya Misri, dhidi ya Pyramids FC, kabla ya kusafiri kwenda Qatar.
Ikiwa watafanikiwa kutoka na ushindi dhidi ya Al-Duhail mnamo Februari 4, watapambana na mabingwa wa Ulaya, Bayern Munich katika nusu fainali.