ZASPOTI

UNAPOZUNGUMZIA walimbwende kutoka nchini India huachi kumtaja mwigizaji na mwanamitindo maarufu ulimwenguni Bipasha Basu, ambae amejizolea sifa nyingi kutokana na urembo wake, umahiri wa kuigiza na kucheza.

Bipasha aliezaliwa Januari 7, 1979, ni mrembo mwenye urefu wa mita 1.72, uzito wa kilogramu 58, nywele ndefu nyeusi na macho makubwa yenye viini vyeusi.

Alianza kutambulika mnamo mwaka 1996 aliposhiriki na kushinda shindano la mitindo liitwalo ‘Godrej Cinthol Supermodel’ na baadae akaendelea na kazi yake hiyo ambayo ilimpatia umaarufu kutokana na urembo wake.

Kutokana na ushindi huo Bipasha alichaguliwa kuiwakilisha India kwenye mashindano ya dunia ‘Ford Models Supermodel’ yaliyofanyika huko Miami, ambayo yalizidi kumtambulisha ulimwenguni na wengi kuvutiwa nae sambamba na kutaka kufanya nae kazi mbali mbali.

Alianza kuonekana katika kurasa za mbele za majarida mbali mbali, pia kufanya kazi na kampuni za mitindo zenye kuuza na kutangaza mavazi tofauti kama vile ‘Calida’.

Kutokana na urembo, mvuto alionao pamoja na umahiri katika kazi yake ya mitindo, Bipasha alianza kupokea ofa za kutakiwa aingie kwenye tasnia ya filamu za kihindi ambapo mnamo mwaka 2001alianza kuigiza filamu ya kwanza iitwayo ‘Ajnabee’, ambayo ilimpatia Tuzo ya mchezaji (dancer) bora wa kike.

Mnamo mwaka 2002, alipewa jukumu la kwanza la kuongoza la filamu iitwayo ‘Raaz’ ambayo ilimpatia tuzo ya mwigizaji Bora.

Baadae alipata mafanikio zaidi katika kuigiza filamu za vichekesho kama vile ‘No Entry’ iliyotoka mwaka 2005 na Phir Hera Pheri  ya 2006.

Pia Alipokea sifa nyingi kutokana na umahiri wa kuigiza filamu za kimapenzi miongoni mwao ni ‘Bachna Ae Haseeno’ ya mwaka 2008.

Sambamba na hilo Bipasha pia alipata sifa nyingi katika juhudi zake za kuigiza filamu za kutisha miongoni mwao ni ‘Aatma’ iliyotoka mwaka 2013.

Mbali na filamu za Kihindi, Bipasha pia ameonekana katika movie mbali mbali za kiengereza kama vile ‘The Lovers’ iliyotoka mwaka 2015 na ‘Singularity’ ya 2012.

Mrembo huyo amepokea tuzo tofauti kutokana na umahiri wake wa kuigiza miongoni mwao ni tuzo za ‘GIFA Awards’, ambapo alitajwa kama muigizaji bora wa mwaka 2007.

Ili kuutengeneza urembo na kueka sawa muonekano wake, Bipasha ni mrembo anaependa kufanya mazoezi ya viungo.

Hivyo anaitumia nafasi yake kushajihisha wanawake juu ya suala zima la mazoezi ya mwili, ambapo mnamo mwaka 2005, alitoa DVD yake ya kwanza ya mazoezi ya mwili, iliyoitwa ‘Bollywood Bodies’.

Aidha, mnamo mwaka 2010, alitoa DVD yake nyengine iitwayo ‘Love Yourself, Fit & Fabulous You’, ambayo ilisisitiza juu ya kuwa mkakamavu, mwenye afya, na kujipenda mwenyewe.

DVD hiyo ilikuwa na utaratibu wa siku 60 za kupunguza uzito, pamoja na mazoezi ya kutengeza sauti kwa waimbaji (sauti laini).

Pia alikuwa balozi wa kampuni ya ‘Sugar Free’, ambayo ilimsaidia kuuza na kusambaza DVD zake za mazoei ya mwili.

Hiren Gada, Mkurugenzi wa ‘Shemaroo Entertainment’ alisema, “mtu mashuhuri kama Bipasha Basu, anaamini kabisa kuwa ni mwenye afya na shauku ya ukakamavu wa mwili ambae ni mfano wa kuigwa na wengine.

Mnamo Septemba 2011 Bipasha alizindua DVD yake ya pili ya mazoezi ya mwili iitwayo ‘Break Free’, ambapo mnamo mwaka 2014, video zake nyingi za mazoezi zilitolewa bure kupitia mtandao wa ‘YouTube’ unaopatikana kwa jina la ‘Shemaroo Good Health 24/7’ yenye wanachama (Subscribers) zaidi ya milioni 1.

Urembo wa mlimbwende huyo ulizidi kuwavutia wengi siku hadi siku ulimwenguni, ambapo mnamo mwaka 2011, katika takwimu zilizofanywa na kituo cha ‘The Times of India’ alishika nafasi ya 8 kwenye wanawake 50 wenye mvuto zaidi na mwaka 2012 kushika nafasi ya 13, na kupanda hadi wa 7 mnamo mwaka 2013.

Bipasha ambae ni mzaliwa wa Delhi na kukulia Kolkata, ametoka katika familia ya Kibengali, ambapo baba yake Hirak Basu ni muhandisi wa serikali na mama yake Mamta Basu ni mama wa nyumbani, pia ana dada wawili ambao ni Bidisha na Vijaya.

Mnamo mwaka 1996-2002 Bipasha alikuwa kwenye uhusiano wa kimapenzi na muigizaji Dino Morea, pia alikua ni mtu wakaribu na nyota wafilamu za kihindi John Abraham kutoka mwaka 2002-2011.

Mnamo Aprili 30, 2016 Bipasha alifunga ndoa na muigizaji mashuhuri Karan Singh Grover.

Wanandoa hao wameweka wazi juu ya mipango yao ya kuanzisha familia, na kusema kwamba kuhusiana na suala la kupata mtoto wanamtegemea Mungu na ikitoke kutopata wao wenyewe basi watachukua wa kulea.

Bipasha katika mahojiano yake na kituo cha ‘Navbharat Times’ alisema, “wacha tusubiri hatma ya Mungu alivyotupangia, na hata ikitokea hatukupata mtoto wetu, ni sawa kwani kuna watoto wengi katika nchi hii, tunaweza kuwatunza pia”.

Bipasha amejizolea umaarufu sehemu nyingi duniani ambapo kwenye ukurasa wake wa instagramu unaonesha ana wafuasi zaidi ya milioni 8.