ZASPOTI

KWA hapa nchini Tanzania, nyota wa muziki wa kizazi kipya, Nasibu Abdul maarufu kama Diamond Platnumz ndiye anayetajwa kama msanii tajiri kulinganisha na wasanii wengine. Pengine ni lebo yake ya WCB kuwa juu, labda pia ni kwa vile amewekeza fedha kwenye majumba na miradi mbalimbali kama ya Wasafi Media, mbali na shoo anazopata kila uchao ndani na nje ya nchi pamoja na matangazo chekwa aliyonayo yanayomuingizia mkwanja wa maana.
Lakini sasa licha ya Diamond kuonekana tajiri, unaambiwa kwa Jose Chameleone anasubiri kwani msanii huyo wa Uganda ambaye majina yake kamili ni Joseph Mayanja na aliyezaliwa miaka 40 iliyopita anatajwa kuwa na ukwasi unaotisha.


Inaelezwa kuwa Chameleone ndiye anayeongoza kwa utajiri miongoni mwa wanamuziki nchini Uganda akikadiriwa kuwa na utajiri wa zaidi ya Sh1.5 bilioni za Tanzania.
Aidha anamiliki mijengo ya bei mbaya ya kukodisha (apartments) iitwayo Daniella Villas jijini Kampala na studio yake iitwayo Leon Island. Takwimu nyingine za kifedha zinamtaja mwimbaji huyo wa AfroBeat kuwa na utajiri wa zaidi ya Dola 5 milioni za Marekani (sawa na Sh11.5 bilioni).
Katika orodha ya mali zake pia anamiliki ufukwe uitwao Coco Beach uliopo Barabara ya Entebbe nchini humo.


Chameleone pia ana mikataba minono na kampuni zinazomtumia kutangaza bidhaa na huduma zake katika taifa hilo la Afrika Mashariki. Moja kati ya mikataba iliyomtajirisha ni ile ya kampuni za simu za MTN na Android.
Pia mkali huyo aliyezaliwa April 30, 1979 inaelezwa anavuta mkwanja mingine kupitia fani yake ya muziki, kwani si mgeni masikioni mwa mashabiki na wapenzi wa muziki Afrika Mashariki na Kati – kwa kazi zake zilizowahi na zinazoendelea kubamba hewani.

ALIPOANZIA

Chameleone alianza muziki mwaka 1996, kipindi hicho akiwa ‘DJ’ katika ukumbi wa usiku wa Missouri uliopo Kampala.
Moja kati ya nyimbo za kwanza ulikuwa wa ‘Bageya’ aliomshirikisha msanii kutoka Kenya, Redsun.
Albamu yake ya kwanza ilitolewa nchini Kenya mwaka 1999. Tangu wakati huo aliachia albamu kadhaa zikiwa pamoja na Bageya ya 2000, Mama Mia ya 2001, Njoo Karibu wa 2002, The Golden Voice ya 2003, Mambo Bado ya 2004 na Kipepo ya 2005.


Aidha alishirikiana kufanya kazi na mwanamuziki mwenzake Bebe Cool, lakini baadaye waliibuka kuwa na upinzani mkali.
Mtindo wa muziki anaocheza Chameleone ni mchanganyiko wa utamaduni wa Kiganda, rhumba ya kati ya Afrika, zouk na ragga.
Jose Chameleone ni mwanachama wa Jamii ya Mwanamuziki, muungano wa wanamuziki ambao hutumia umaarufu na mali zao kusaidia kuondoa umaskini na kujenga kampeni za mwamko wa kupambana na Virusi Vya Ukimwi (VVU). Amezitembelea nchi nyingi za ng’ambo kufanya maonyesho zikiwemo Marekani, Uingereza na Sweden.

KIPEPEO HATARI

Kama kuna wimbo wake uliowahi kuwashika mashabiki, basi ni Kipepeo uliokuwa haukauki vinywani mwa watu wazima pamwe na watoto wadogo wakisikika wakitamka “Kipepo, Kipepeo”- wimbo ambao ulitungwa na kuimbwa na nyota huyo.
Aidha alifanya ‘kufuru’ baada ya kuachia vibao vya Jamila, Bei Kali, Mama Rhoda na vingine vingi vilivyomuongezea umaarufu zaidi. Ngoma zake zingine ambazo zimewahi kutikisa kwenye soko la muziki barani Afrika ni Wale Wale, Nkoleki, Vale Vale, Dorotia, Tubonge, Agatako na Pam Pam na unaambiwa mpaka mwaka 2013 tayari alikuwa na albamu 12.


AVUNJA REKODI

Miongoni mwa matukio yaliyowahi kumpa umaarufu mkubwa ni kuvunja rekodi ya kuingiza mashabiki wengi kwenye Uwanja wa Kriketi wa Lugogo nchini Uganda. Katika onyesho hilo lililopachikwa jina la Tubonge Live, takribani mashabiki 40,000 walizama ndani kushuhudia.
Licha ya kufanya vizuri nchini mwake, kazi za Chameleone zimekuwa zikitesa nje ya mipaka ya nchi hiyo.

ANAISHI KISHUA

Kutokana na utajiri alionao amekuwa akiishi maisha ya kifahari ambapo mwenyewe alithibitisha kuwa muziki unalipa.
Kali zaidi ni pale aliponunua jozi mbili za viatu vya kisasa vilivyomgharimu kiasi cha zaidi ya Sh40 milioni.
Chameleone na familia yake wanaishi kwenye jumba lao la kifahari lenye thamani kubwa nje kidogo ya Jiji la Kampala. Aidha anamiliki Coco Beach, iliyopo ufukweni mwa Ziwa Victoria, kukiwa na vivutio vya burudani vyenye thamani zaidi ya Sh27 milioni.
Jose pia anamiliki magari ya kifahari aina ya Cadillac Escalade, BMW, Premio, Toyota Ipsum, Landcruiser VX, Mercedes Benz yenye thamani Sh270 milioni.

MIRADI MINGINE

Chameleone amewekeza kwenye miradi mingine mikubwa inayomuongezea kipato ikiwa ni pamoja na kumiliki mjengo wa kupangisha ‘apartment’ katika mji wa Arizona nchini Marekani, jumba la kifahari katika vilima vya Sekuku jijini Kampala na nyumba nzuri aliyoinunua kwa bei ‘ndefu’ mjini wa Kigali, Rwanda.


Mwaka 2013 alitajwa kuwa mmoja kati ya wasanii sita matajiri Afrika. Awali wasanii Bebe Cool na Navio walijitangaza kuwa ndio matajiri nchini Uganda.
Chameleone baada kusikia habari hiyo ndipo alipoibuka na kuanza kuanika mali zake kwa kilichodaiwa kukerwa zaidi aliposikia watu wanasema kuwa aliongopa kutamka kuwa alimpa mkewe gari aina ya Range Rover katika sikukuu ya Wapendanao.


“Haijalishi mimi kumnunulia Daniella Range Rover, lakini yeye ana lake na langu lipo. Watu wanapaswa kuamini kuwa mimi ni mwanamuziki tajiri na mwenye mali kibao,” alijigamba Chameleone.

TUHUMA NZITO

Jinsi mafanikio yake yalivyokuwa yakitiririka mithiri ya maji mtoni, nguli huyo aliwahi kutuhumiwa kwamba hutumia nguvu za giza katika kutengeneza utajiri alionao hatimaye kupandisha umaarufu wake. Mahasimu wake walidai kuwa utajiri na umaarufu wake barani Afrika umetokana na ndumba.
Aliyekuwa wa kwanza kumtuhumu Chameleone kutumia nguvu za giza ni mkali wa muziki wa ragga, Badman Denzo. Badman alisema Chameleone amekuwa ‘akinyunyiza’ ili kufanikisha malengo yake kimuziki.


Nyota huyo alidai kuwa Chameleone amekuwa akitembelea Tanzania mara kwa mara kwa lengo la kukutana na waganga wake. Badman aliyasema hayo wakati alipokuwa akihojiwa na kituo cha televisheni cha NBS.
Nyota huyo aliyewahi kutamba na kibao cha Big Mouth By Far alimtaja Chameleon pale alipoambiwa amtaje msanii mmoja anayetumia nguvu za giza. “Nina uhakika Chameleone anatumia uchawi, huwa anapata mambo hayo kutoka Tanzania, niliwahi kumkuta Dar es Salaam,” alidai Denzo.
Chameleone aliposikia shutuma hizo alikanusha vikali huku akisisitiza kuwa ni jitihada zake binafsi ndio msingi wa mafanikio.


Chameleone ambaye ni kaka wa mastaa wa muziki Uganda, Palaso na Weasel, alisema ni muumini mzuri wa dini ya Kikiristo, si rafiki wa shetani na kuongeza kuwa uchawi hauna ‘dili’ kwake.
Chameleone aliwahi kuwepo kwenye orodha ya wanamuziki matajiri Afrika akiwa ni mwimbaji pekee aliyeiwakilisha Uganda kwenye orodha hiyo.
Chameleone alifanya onyesho kubwa Desemba 2014, ambalo kiingilio kilikuwa Sh1 milioni za Uganda. Katika onyesho hilo gari lake jipya aina ya Range Rover la mwaka 2013, lilionekana kwa mara ya kwanza.


Pia Chameleone alinunua jozi moja ya viatu kwa kulipa Dola12,500. Wakati huohuo wengine wakadai eti anajionyesha kuwa anazo, lakini Chameleone alisema ameamua ‘kuizawadia’ miguu yake. Alifafanua kuwa anarudisha shukran kwa miguu yake kwa kusimama naye na kumwezesha kufika alipo sasa. Mwimbaji huyo wa ‘’Wale Wale, waliobarikiwa na Mungu’’, alisema siyo majivuno kamwe, bali ni njia yake ya kumshukuru Mungu kwa kumjalia na kumpa uwezo kama huo.


Wimbo huo tayari umetazamwa na watu zaidi ya milioni moja na laki tatu katika mtandao wa Youtube. Alipokuwa ziarani nchini Kenya aliwaacha watu vinywa wazi baada ya kuweka mtandaoni picha ya viatu vyake aina ya Nike Air Mag ambavyo jozi hiyo alinunua kwa Dola 12,500 za Kimarekani.

AJALINI
Mwenyewe alisema anajipa raha, ‘’jifurahishe ungali hai’’, Chameleone alijigamba.
Chameleone alikumbusha kuwa miaka zaidi ya minane iliyopita angekuwa kiwete kutokana na ajali mbaya. “Sasa nimepona na pesa ziko kwanini nisiishukuru miguu yangu?,” akasema.
Ikumbukwe kwamba Jose Chameleone alijirusha kutoka ghorofa ya tatu katika hoteli ya Impala jijini Arusha, na kusababisha kuumia vibaya ikiwa ni pamoja na kuvunjika miguu yote.


Walinzi wa hoteli hiyo walikimbilia eneo aliloangukia baada ya kusikia kishindo, wakamkuta akiwa hawezi kuinuka. Hata hivyo, haikueleweka mara moja sababu zilizomfanya mwanamuziki huyo kujirusha. Baada ya tukio hilo wenyeji wake ambao walikuwa ni Clouds FM, waliokuwa wamemualika kwa ajili ya shughuli ya Fiesta ya Tanga, walilazimika kufanya utaratibu wa kumpeleka hospitali.
Taarifa zilipomfikia baba yake huko Uganda, alikodi ndege ambayo ilitumwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (Kia), kwa ajili ya kumbeba C akapelekwa kwao Uganda ambako alilazwa.


Kuumia kwake kulisababisha ashindwe kufanya onyesho katika tamasha hilo, ambako kulikuwa na wasanii wengi wa Tanzania.
Chameleone anasisitiza kuwa baada ya kumiliki nyumba, magari na akaunti iliyonona benki, sasa ana ndoto za kumiliki chopa (helikopta). Sababu ni kwamba amekuwa akikodi mara kadhaa kwenda katika matamasha au kama alivyofanya wakati anamuoa mkewe, Daniela.

FAMILIA

Chameleone anaweza kuonekana jeuri na mtata mbele ya mashabiki wake, lakini ni baba anayeipenda familia, anayewajibika kuiweka katika mazingira mazuri kadri awezavyo. Chameleone ana mke na watato wanne. Wa kwanza ni wa kike aitwaye Ayla aliyempata wakati akiwa kwenye mahusiano na Dorotia. Katika ndoa yake na Daniella, wamepata watoto watatu, Abba, Alfa Mayanja na Alba.

SIASA

Jose Chameleone aliingia katika siasa baada ya kutangaza kuwania umeya wa Jiji la Kampala ili kushindana na Erias Lukwago.
Hivi karibuni alijiunga na vuguvugu la harakati za nguvu za watu “Peoples Power Movement” – kundi linaloongozwa na mwanamuziki mwenzake aliyeibukia katika siasa, Bobi Wine.