NA MWANDISHI WETU
KASI ya mfumko wa bei wa mwaka ulioishia Disemba 2020, imeendelea kupungua na kufikia asilimia 0.5, ikilinganishwa na asilimia 1.0 kwa mwaka uliomalizikia Novemba 2020.
Hayo yameelezwa na Mkuu wa Kitengo cha Takwimu za Bei Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Khamis Abdulrahman Msham, alipokuwa akiwasilisha ripoti ya mfumko kwa mwezi Disemba huko Mazizini.
Alisema, kiwango cha mfumko wa bei ya vyakula na vinywaji visivyo na vilevi kilipungua hadi asilimia 0.9 mnamo Novemba 2020 kutoka asilimia 1.5 huku faharisi za bei zikifikia 112.9 mwezi Disemba ikilinganishwa na 112.3 mwaka 2019.
Bidhaa zilizochangia kupungua kwa kiwango cha mfumko wa bei wa mwaka ni mchele wa mapembe (3.4%), mchele wa Mbeya (6.7%), unga wa sembe (6.7%), saruji (17.0%), mafuta ya taa (25.9%), petroli (12.7%) na dizeli (18.7%).
Mchumi kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BOT), Ulrick Mbumbuvi, alisema, kuendelea kupumua kwa mfumko kumechangiwa na kuwepo kwa bidhaa za kutosha kwenye masoko na uzalishaji mzuri.
Aidha, alisema, kuwepo kwenye tarakimu moja, ni njia bora ya kuwavutia wawekezaji kwa ajili ya kuwekeza nchini kwa ajili ya maendeleo ya taifa.
Mkurugenzi wa Idara ya Takwimu za Kiuchumi Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Abdulrauf Ramadhan, alisema, mfumko wa bei wa mwaka mzima wa 2020, uliofikia asilimia 3.4 kutoka asilimia 2.7 mwaka 2019.
Alisema, hiyo ni sawa na ongezeko na asilimia 0.7 ambalo lilisababishwa na kupanda kwa bidhaa za vyakula na zisizokuwa za vyakula.
Alisema kati ya bidhaa hizo, 204 ziliongezeka bei ambazo za vyakula zilikuwa 79 na zisizokuwa za vyakula zilikuwa 125.
Alisema, katika bidhaa zilizoshuka bei zilikuwa 86 zikiwemo za vyakula 37 na 125 zisizokuwa za vyakula bidhaa 53 hazikuwa na mabadiliko ya bei.