NA SAIDA ISSA, DODOMA

WASTANI wa mfumuko wa bei wa Taifa kutoka mwezi Januari hadi Desemba ,2020 umepungua hadi asilimia 3.3 kutoka asilimia 3.4 Mwaka 2019 kutoka Januari hadi Desemba.

Hayo yamebainishwa jana jijini hapa na Mkurugenzi wa Ruth Minja wakati akiongea na waandishi wa habari Kuhusu hali ya mfumuko wa Bei wa Taifa.

Alieleza kuwa wastani wa Mfumuko wa bei wa bidhaa za vyakula umeongezeka hadi asilimia 5.0 mwaka 2020 kutoka asilimia 4.3 mwaka 2019.

Mkurugenzi huyo aliongeza kuwa kwa upande wa bidhaa zisizo za vyakula kwa mwaka 2020 wastani wake umepungua hadi asilimia 2.8 kutoka asilimia 4.0 ilivyokuwa mwaka 2019.

“Wastani wa Mfumuko wa bei usio jumuisha bidhaa za vyakula na nishati umepungua pia hadi kufikia asilimia 2.3 mwaka 2020 kutoka asilimia 3.0 mwaka 2019,”alifafanua.

Katika hatua nyingine alisema mfumuko wa bei wa Taifa kwa mwaka ulioishia mwezi Desemba 2020 umeongezeka hadi asilimia 3.2 kutoka asilimia 3.0 kwa mwaka ulioishia mwezi Novemba 2020.

“Hali hii inamaanisha kuwa kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma kwa mwaka ulioishia mwezi Desemba 2020 imeongezeka kidogo ikilinganishwa na kasi iliyokuwepo kwa mwaka ulioishia mwezi Novemba 2020,”alifafanua.

Aliongeza kuwa kuongezeka kwa mfumuko wa bei ulioishia mwezi Desemba 2020 kumechangiwa na kuongezeka kwa bei za baadhi ya bidhaa za vyakula na zisizo za vyakula kwa kipindi kilichoishia mwezi Desemba 2020 zikilinganishwa na bei za mwezi Desemba 2019.

“Baadhi ya bidhaa za vyakula zilizoongezeka bei kwa mwezi Desemba 2020 zikilinganishwa na bei za mwezi Desemba 2019 ni pamoja na nyama kwa silimia 3.1,samakai wabichi kwa asilimia 15.6,mayai kwa asilimia 3.0 na dagaa kwa asilimia 13.2,”alisema na kuongeza;

Nyingine ni mafuta ya kupikia asilimia 9.0 ,matunda kwa asilimia 16.9,maharage asilimia 6.2,choroko asilimia 12.0 ,viazi mviringo kwa asilimia 5.5 na mihogo kwa asilimia 13.5,”alisema.

Mbali na hayo alizungumzia baadhi ya bidhaa zisizo Za vyakula zilizoongezeka bei  kwa mwezi Desemba 2020 zikilinganishwa na bei za mwezi Desemba 2019 ni pamoja na nguzo za kiume kwa asilimia 3.9 ,nguo za wanawake kwa asilimia 3.3 ,viatu vya wanaume asilimia 2.5 na viatu vya wanawake asilimia 2.0.