NA SAIDA ISSA, DODOMA

WASTANI wa mfumuko wa bei wa Taifa kutoka mwezi Januari hadi Desemba ,2020 umepungua hadi asilimia 3.3 kutoka asilimia 3.4 Mwaka 2019 kutoka Januari hadi Desemba.

Hayo yamebainishwa jana jijini hapa na Mkurugenzi wa Ruth Minja wakati akiongea na waandishi wa habari Kuhusu hali ya mfumuko wa Bei wa Taifa.

Alieleza kuwa wastani wa Mfumuko wa bei wa bidhaa za vyakula umeongezeka hadi asilimia 5.0 mwaka 2020 kutoka asilimia 4.3 mwaka 2019.

Mkurugenzi huyo aliongeza kuwa kwa upande wa bidhaa zisizo za vyakula kwa mwaka 2020 wastani wake umepungua hadi asilimia 2.8 kutoka asilimia 4.0 ilivyokuwa mwaka 2019.

“Wastani wa Mfumuko wa bei usio jumuisha bidhaa za vyakula na nishati umepungua pia hadi kufikia asilimia 2.3 mwaka 2020 kutoka asilimia 3.0 mwaka 2019,”alifafanua.