KWA mara nyengine tena Zanzibar imeandika historia mpya miongoni mwa nchi nyingi za Afrika kwa kumchagua msimamizi mkuu wa shughuli za serikali kuwa mwanamke.

Kwa hakika moja na nafasi kubwa nyeti ya kiutendaji katika serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, ni Katibu Mkuu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi, ambapo kwa mara ya dhamana hiyo amepewa mwanamke.

Kwa mujibu wa sheria ya utumishi wa umma ya mwaka 2011, inamtaja Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi kama msaidizi mkuu wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi katika utumishi wa umma.

Wapo wengi waliokuwa wakitajwa kuwa na sifa za kuchukua nafasi hiyo, lakini Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, ameonesha imani hiyo kwa kumteua Mhandisi Zena Ahmed Said.

Mhandisi huyo anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Dk. Abdulhamid Yahya Mzee, ambaye ameitumikia nafasi hiyo kwa muda mrefu, hadi alipostaafu rasmi mnamo Disemba 31 mwaka 2020.

Kwa hakika Dk. Abdulhamid kwa kipindi chote amefanyakazi nzuri wakati alipokuwa kwenye nafasi hiyo, bila shaka mrithi wake atayaendeleza vyema kwa ajili ya maslahi ya wananchi wa Zanzibar.

Wengine hatushangai sana Dk. Mwinyi kumteua Mhandisi Zena kuchukua nafasi hiyo kwasababu tayari alikwisha eleza wakati alipokuwa kwenye kampeni za kusaka urais ambapo alieleza teuzi zake zitazingatia uwezo wa kiutendaji, uwajibikaji na elimu.

Hata hivyo, wakati alipokuwa kwenye kampeni za kusaka kura na kukutana na makundi maalum hasa ya wanawake alisema kuwa atawapa nafasi za kutosha, hivyo, nafasi hiyo kubwa kupewa Mhandisi Zena ni utekelezaji wa ahadi za rais wetu.

Pengine Mhandisi Zena si mashuhuri sana kwenye siasa za Zanzibar, hata hivyo tunaamini anaweza kuendana na kasi kubwa ya serikali ya awamu ya nane chini ya Dk. Hussein Mwinyi, hasa ikizingatiwa kwa umri wake unaruhusu kuwa na nguvu za kufanya hivyo.

Kwa nafasi yake Mhandisi Zena anaweza kuwa mhimili mkubwa wa kuhakikisha anafanikisha ndoto na malengo ya Dk. Hussein Mwinyi hasa kupiga vita uzembe, ubadhiri na wizi kwenye sekta ya umma.