Dk. Mwinyi apania kuinua hadhi ya michezo

Sanaa, burudani kupata msukumo mpya

NA AMEIR KHALID

MIAKA 57 ya Mapinduzi ya Zanzibar, ambayo leo hii tunasherehekea, tukiwa na fahari kubwa ya kujivunia mafanikio mengi ambayo yamepatika ndani ya miaka hiyo.

Kila mmoja atakuwa shahidi wa haya, kwani miaka mingi imepita tangu Zanzibar kupata uhuru wake kutoka kwa ukoloni wa kisultani, ambao kabla ya hapo mambo mengi hayakuwa rahisi kuyapata.

Mbali na maendeleo mengi ambayo yamepatikana kwenye sekta tofauti, pia katika michezo huwezi kuiacha mbali kwani nayo pia imepiga hatua kubwa na kumekuwa na mabadiliko mengi ambayo yamepatikana katika kipindi cha miaka 57 ya mapinduzi.

Tofauti na miaka 10 iliyopita, mwaka huu miaka hii 57 ya mapinduzi sherehe zake zitanoga zaidi kwa kuwa na rais mpya wa awamu ya nane ambaye ni Dk. Hussein Ali Mwinyi.

Dk. Mwinyi ameingia madarakani mwezi Novemba mwaka jana baada ya kushinda uchaguzi mkuu uliofanyika mwezi Oktoba, na hatiamae kushinda kwa kishindo kikubwa kilichovunja rekodi ya uchaguzi Zanzibar.

Katika siku chache tangu Dk. Mwinyi ameingia madarakani tayari ameanza kuonesha matumaini ya Wazanzibari, kutokana na aina ya uongozi wake wa kutovumilia ubadhirifu kwa watendaji wa serikali.

Wakati akiwa katika mikutano ya kampeni Dk. Mwinyi aliahidi mambo mengi sana katika sekta ya michezo na sanaa, na hata pale alipomaliza kula kiapo kuwa rais wa Zanzibar, anaendelea na msimamo wake kuwa atatekeleza ahadi zake zote alizoahidi.

Hivyo basi wakati tunaadhimisha miaka 57 ya mapinduzi ya Zanzibar, imani ya wazanzibari wengi wakiwemo wanamichezo kupata mafanikio makubwa katika sekta hiyo.

Wakati miaka 57 ya Mapinduzi yanaadhimishwa leo hakika wanamichezo wengi hivi wana imani ya kuwepo mabadiliko makubwa sana ya sekta ya michezo, kwa kuona michezo, sanaa na utamaduni, vinapiga hatua na kuleta maendeleo kwa nchi na wanamichezo wenyewe.

Hili linatia moyo zaidi baada ya ahadi za kweli ambazo Dk. Mwinyi aliziahidi wakati wa kampeni za kuomba kuchaguliwa kuingia Ikulu.

Katika ahadi hizo Dk. Mwinyi alisema atafanya juhudi zote ili kuwahamasisha wafanyabiashara wakubwa Zanzibar kudhamini michezo pamoja na kulitafutia ufumbuzi suala la migogoro ya vyama vya michezo.

Dk. Mwinyi aliahidi kuondosha migogoro ya muda mrefu katika vyama vya michezo jambo ambalo limezoretesha na kurejesha nyuma sekta ya michezo hapa Zanzibar.

Aidha Dk. Mwinyi aliahidi kuwashirikisha vya kutosha wafanyabiashara hao ili waweze kudhamini ligi kuu zote za Zanzibar na si mpira wa miguu peke yake.

Pamoja na hayo Dk. Mwinyi alisema atahakikisha serikali inatenga fungu maalum kwa ajili ya kukuza michezo.

Mbali na hayo Dk. Mwinyi alisema, atahakikisha kuwa anajenga vyama imara vya michezo ambavyo vitakuza michezo nchini.

Sambamba na hayo, Dk. Mwinyi alisema kila mmoja akitimiza majukumu yake kwa kuona changamoto zote zinazoikabili sekta ya michezo basi michezo ya Zanzibar itakuwa.

Alisema kwa upande wa serikali kuna majukumu manne makubwa, kwanza ni sera ambapo alisema lazima kuwe na sera nzuri ya michezo.

Jukumu la pili la serikali kuangalia sheria ya michezo ya mwaka 2010, na kama kuna mambo ambayo yamepitwa na wakati, wakati umefika wa kutizama sheria hiyo na kuirekebisha ili ijibu changamoto zinazokabili michezo.

“Eneo la tatu uwezeshaji, serikali inajukumu la kuiwezesha michezo, tukiacha michezo ijiendeshe yenyewe lazima kutokee mikwamo, hivyo ipo haja ya kuhakikisha serikali inawezesha michezo,” alisema.

Katika hilo Dk. Mwinyi atajenga mazingira mazuri ya michezo ikiwa ni pamoja na kuhimiza michezo katika skuli.

Vipaji lazima viibuliwe mapema katika skuli, hivyo lazima skuli za Zanzibar ziwe na mazingira mazuri ya vijana kuweza kucheza michezo inakayosaidia kuibua vipaji mapema.

Dk. Mwinyi alisema lazima kuwe na viwanja vya michezo katika maeneo yote ambayo wananchi wanaishi ukianzia shehia, wilaya na mikoa.

“Usipokuwa na viwanja vya michezo huwezi kuibua vipaji kwa hivyo hilo ni jukumu la serikali zote kuanzia chini mpaka juu kuhakikisha kwamba viwanja vizuri kwa watu kufanya michezo ili kuendeleza michezo tulokuwa nayo,” alisema.

Kuhusu vituo vya kulea vipaji kwa vijana (sports academy) alisema anaamini kukiwa na vituo hivyo, michezo itaendelezwa vizuri kwa sababu wengi wa wanamichezo wanachelewa kuanza kutokana na kulelewa mapema.

Dk. Hussein Ali Mwinyi aliahidi anajenga viwanja vya kufurahishia watoto kila eneo, ili kuepuka msongamano katika maeneo ya mjini.

 “Haiwezekani siku ya sikukuu ya mfungo mosi au mfunguo tatu watoto wote waende Mnazimmoja au Fumba, hili ni jambo la kulifanyia kazi na kutambua kuwa, tukiwa na uwanja wa watoto katika maeneo tofauti peke yake ni utalii kwani tutawahudumia wandani na wa nje,” alisema.

Hivyo alibainisha kwamba atatahakikisha maeneo yote yanakuwa na viwanja hivyo na kutakuwa hakuna haja watu wote kukutana mjini ili kupunguza msongamano.

Kwa upande wa sanaa alisema wasanii wanafanya kazi kubwa hivyo ni vyema atawapo kipao mbele ili kazi zao ziinuwe uchumi.

Alisema atasaidia wasanii kwani kuna vipaji vingi ambavyo vinahitaji kuendelezwa.

Tayari mafanikio ya michezo ndani ya awamu hii ya nane yameanza kuonekana, mfano wa hivi karibuni ni mashindano ya Yamle Yamle ambapo siku ya fainali Dk. Mwinyi alikuwa mgeni rasmi na kukabidhi zawadi kwa washindi.

Hatua hiyo ya Dk. Mwinyi kuwa mgeni rasmi kuliamsha shamra shamra nyingi kwa mashabiki ambao walijazana kwa wingi katika dimba la Amaan, hatua ambayo inatoa taswira kuwa wanamichezo wanamkubali Dk. Mwinyi.

Pia nyota nyingine ya matumaini kwa awamu ilijitokeza wakati timu ya Mlandege ilipokuwa inataka kwenda nchini Tunisia katika mashindano ya klabu bingwa, ambapo wafanya biashara mbali mbali walifika Ikulu kutoa michango yao kwa Dk. Mwinyi na hatimae timu hiyo kufanikisha safari ya Tunisia.