Mfuko wa Uwezeshaji wananchi kiuchumi wabeba matumaini ya wanyonge

Wengi wajiajiri, wapata kipato kupitia mikopo nafuu

Dk Hussein ataka vijana kuichangamkia

NA HUSNA MOHAMMED

IKIWA jana wananchi wa Zanzibar wanashrehekea miaka 57 ya Mapinduzi matukufu ya Zanzibar yapo mengi ya kujivunia.

Miongoni mwa hayo na serikali kutafakari kuona namna gani wananchi wanaweza kusaidiwa kiuchumi ili kwenda sambamba na dhana halisi ya mapinduzi kuona wannachi wanaishi maisha mazuri na kujitegemea.

Ndio maana Serikali ya awamu ya saba iliyokuwa chini ya Rais mstaafu ikaona ipo haja ya kuanzisha mfuko maalumu wa kuwawezesha wananchi kiuchumi kwa kuwapa miko ya riba ndogo kabisa na kuanzisha miradi mbalimbali katika jamii.

Mfuko wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Zanzibar ni Taasisi ya utoaji wa huduma za mitaji kwa wajasiriamali wadogo kwa lengo la kuwaendeleza kiuchumi na kimaisha kiuchumi itakayowapatia kipato cha kujikimu kimaisha yao ya kila siku.

Aidha, uwepo wa Mfuko huu ni Mkakati mmojawapo wa Serikali wa kupunguza tatizo la ajira na umaskini katika jamii hapa Zanzibar.

Mfuko wa aina hii hautakiwi kupewa fedha za kutolea mikopo, badala yake hutumia pesa za kutolea mikopo kutokana na marejesho ya mikopo unayoitowa (Revolving loan fund) bali hutumia fedha ilizonanzo za kutolea mikopo.

Zanzibar, kama zilivyo nchi nyingi zinazoendelea, sehemu kubwa ya wananchi wake ni watu masikini, hususan akinamama.

Wananchi hawa hukosa huduma za kifedha ambazo ni muhimu sana katika kujipatia mitaji watakayoitumia kufanya shughuli za uzalishaji mali, na hivyo kuwa ni sehemu ya ajira kwao.

Kwa bahati mbaya sana, wananchi walio masikini, hususan wa vijijini wameachwa nyuma katika kuwapatia huduma za fedha licha ya jitihada kubwa inayofanywa na Serikali pamoja na taasisi zisizo za serikali kuanzisha SACCOS, VICOBA na UPATU.

Hivyo, basi Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, katika uongozi wa awamu ya saba cha kipindi cha miaka minane chini ya Rais mstaafu Dk Ali Mohamed Shein, ulianzisha mfuko huo kwa lengo la kuwataka wanawake kuunda vyama vya ushirika na uwekezaji jinsi ya kuwainua wananchi kiuchumi.

Miongoni mwa mambo yaliyosaidia sana katika kupunguza umasikini na kuleta ajira nchini ni suala la uanzishaji wa vyama vya ushirika.

Kwa sasa imani kwa vyama vya ushirika imeongezeka mara dufu na Serikali imezingatia na kuwashajihisha wananchi kuanzisha na kuviendeleza vyama hivyo.

Pamoja na mambo mengine lakini Serikali inayoongozwa na Chama cha Mapinduzi ambayo imeifanyia mapitio Sera ya Vyama vya Ushirika na kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Vyama vya Ushirika sambamba na upatikanaji wa takwimu zitakazosaidia kuandaa mipango na kuleta mageuzi katika Sekta ya Ushirika na kuimarisha uchumi wa Taifa.

Ikaonekana kuwa shughuli za kuwawezesha wananchi kiuchumi kupitia Idara hakuleti matokeo chanya na kunapunguza ufanisi, hivyo mwanzoni mwa mwaka 2012, serikali iliyokuwa madarakani ilianza mikakati ya kuhuisha shughuli za Idara hii kwa kuteua Kamati Maalum ya kukusanya Fedha ili kupata fedha nyingi zitakazowanufaishi wananchi wengi zaidi wa Unguja na Pemba.

UANZISHWAJI WA IDARA YA UWEZESHAJI WANANCHI KIUCHUMI

Baada ya kupatikana pesa za kuanzia, ndipo Rais mstaafu Dk. Shein tarehe 21 Disemba, 2013, katika ukumbi wa Zanzibar Beach Resort, akauzindua rasmi Mfuko huu na kuanzia hapo ikawa  sio Idara ya Mikopo tena, bali ni Mfuko wa uwezeshaji wananchi kiuchumi (muwk).

Uzinduzi huu ulikwenda sambamba na shamra shamra za sherehe za  maadhimisho ya miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar ambayoyalifikia kilele chake tarehe 12 Januari, 2014.

Aidha Serikali ilikamilisha Sera ya Maendeleo ya Vyama vya Ushirika na hivi sasa iko hatua ya utekelezaji wake. Sheria ya Maendeleo ya Vyama vya Ushirika Nambari 4 (1986) inafanyiwa mapitio na Rasimu ya Sheria mpya ya Vyama vya Ushirika imeandaliwa na imeshatafsiriwa kwa lugha ya Kiswahili.

Kufanya usajili wa vyama vipya vya ushirika 600 vya uzalishaji (kilimo, mifugo, viwanda vidogo vidogo, uvuvi na huduma) pamoja na SACCOS 50 kubwa ni mambo ambayo yalipewa kipaumbele kwenye mfuko huo.

Serikali wakati huo ilisajili vyama 585 (477 Unguja na 108 Pemba) ambapo kati ya hivyo 566 ni vya uzalishaji na 19 ni vya SACCOS.

Idadi ya wanachama katika vyama hivyo walikuwa ni 10,979 ambapo 9,553 Unguja na 1,426 Pemba. 3,574,750.

Sambamba na hilo, lakini mfuko huo uliziimarisha SACCOS na Asasi Ndogo za Fedha kwa kuzipatia mafunzo ya kitaaluma, uongozi na kuwaongezea mitaji ili ziweze kutekeleza shughuli zake kwa ufanisi kwa lengo la kuongeza ajira;

Aidha Serikali ilitoa mafunzo kwa SACCOS 215 zenye wanachama 12,270 juu ya Uongozi na Mbinu za Kuimarisha Mitaji, Ukaguzi wa Hesabu za Vyama vya Ushirika. Mafunzo hayo yaliwajumuisha viongozi, wanachama, waandishi wa habari na watendaji.

Kupitia mfuko huo yalitolewa mafunzo ya uongozi na uendeshaji wanachama 15,000 wakiwemo viongozi 3,000 na wanachama 12,000 wa vyama vya ushirika na kuvifanyia ukaguzi vyama 3,000 vya ushirika.

Serikali ilihamasisha uundaji wa Vyama Vikuu vitatu vya Sekta ya Kilimo (viwili Unguja na kimoja Pemba). Pia, Chama Kikuu cha Kitaifa cha Kilimo Zanzibar kimeundwa na kimeanza shughuli za kuendeleza kilimo.

UTOAJI WA MIKOPO:

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Idaya ya Uwezeshaji, Wananchi kiuchumi Zanzibar, Suleiman Ali Haji, anasema hadi kufikia Novemba 30, 2020 jumla ya mikopo 3,628   yenye thamani ya shilingi 4,555,798,000 ilikuwa imetolewa katika Shehiya 364 Unguja na Pemba.

Anasema shilingi 1,262,292,000 zilitolewa kisiwani Pemba, wakati Unguja zilitolewa Shilingi 3,293,506,000.

Anaeleza mbali na utoaji wa fedha hizo, Mfuko kupitia Mradi wa Mbogamboga na Matunda umetoa jumla ya mikopo 726 kwa wakulima wa kilimo hicho, akibainisha mikopo 302 yenye thamani ya Shilingi 212,200,000 imetolewa kisiwani Pemba kwa wakulima 2,216, wakati ambapo Unguja imetolewa mikopo  424 yenye thamani ya Shilingi 367,398,000 kwa wakulima  2,462 .

Aidha, anasema asilimia 42 ya wakulima wa kilimo hicho walinufaika na mikopo ya mfuko  huo  unaosimamiwa na Shirika la ‘Feed the future’ na kufadhiliwa na Shirika la Misaada la Marekani (USAID),  huku asilimia 23 wakiwa wafanyabiashara wa aina mbalimbali ikiwemo maduka ya vyakula ya jumla na reja reja, na silimia 35  ni wenye viwanda vidogo vidogo, uchongaji,ufugaji, kazi za mikono na Uvuvi.

UREJESHAJI MIKOPO:

Mkurugenzi Suleiman anasema wastani wa asilimia 96 ya matarajio ya marejesho hayo yamefanyika.

Anasema kuanzia Julai 2014 hadi Novemba 2020, jumla ya shilingi 2,950,058,022 zimerudishwa ambapo shilingi 403,694,005 zimerejeshwa mwaka 2014/2015, shilingi 435,644,500 (2015/2016), Shilingi 413,180,000 (2016/2017), shilingi 462,050,938 (2017/2018), shilingi 524,345,979 (2018/2019), shilingi 539,861,800 (2019/2020), huku jumla ya shilingi 171,280,800 zimekusanywa katika kipindi cha miezi mitano ya 2020/2021.

Anaeleza kuwa Marejesho yameendelea kuwa ya kutia moyo kutokana na sababu mbalimbali, ikiwemo Umakini wa maafisa wa Mikopo Wilayani katika kutathmini maombi ya wanaotaka mikopo.

“Utoaji wa mafunzo ya aina mbali mbali kabla na baada ya mikopo kipindi cha biashara pamoja na kuwepo Ufuatiliaji wa karibu na wa mara kwa mara kwa wateja unaofanywa na maafisa   wa Mikopo   kwa kushirikiana na Masheha wa Shehia zote”, anasema.

Aidha, anasema kuwepo ushirikiano mzuri kati ya watendaji wa Mfuko na wale wa Serikali za Mitaa hususan ngazi ya Wilaya na Shehia pamoja Ushirikiano mzuri na Wakuu wa Wilaya, Maafisa ushirika na watendaji wa Wizara umechangia kuleta ufanisi.

WANUFAIKA WA MIKOPO WAZUNGUMZA

Mtumwa Ali ni miongoni mwa wanufaika wa mikopo, alisema ameshachukua mikopo takriban mara mbili na kwamba alisema umemsaidia sana kimaisha.

“Nimeongezea mtaji wangu wa uanikaji wa dagaa baada ya kupata mkopo shilingi 500,000 awamu ya kwanza na wa pili kima hichohicho ni meshalipa zote na sasa nahesabu faida tu.

Aliwataka wanawake wasiokuwa na kazi kuacha kukaa bure na kuwa tegemezi na hivyo kutumia fursa ya mikopo ili kujiendesha kimaisha.

Nao wanakikundi cha ‘Rabi Salama’ walisema kuwa wamepata mkopo kupitia mfumo huo ambao kwa sasa unaendelea vyema.

“Tulijikusanya kama watu 15 hivi tukaomba mkopo na sasa ushirika wetu unaendelea vizuri”, alisema.

Mapema Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, akitoa hotuba katika ufunguzi wa Baraza la wawakilishi kwa awamu hii ya nane, sambamba na hotuba ya sherehe za Mapinduzi mwaka huu wa 2021, alisema serikali taongeza bajeti kwa vijana ili kuongeza mitaji ya biashara kupitia Mfuko wa uwezeshaji.

“Nawasihi vijana watakaopata mikopo kupitia Mfuko huu pamoja na Mifuko mingine ya uwezeshaji wahakikishe wanaitumia vizuri kwa malengo yaliyokusudiwa na kuirejesha kwa wakati ili wengine nao wapate”, aloisema.

Rais Dk Hussein alisema Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi ni miongoni mwa malengo ya Serikali ya Awamu ya 8 katika kukabiliana na tatizo la umaskini wa kipato unaosababishwa na ukosefu wa ajira.

“Tunaelewa kuwa bado kuna changamoto zinazowakabili wananchi katika kuendesha shughuli za ujasiriamali, ambazo zinahusiana na ukosefu wa mitaji, vifaa, utaalamu wa kutosha wa kuendesha biashara na utafutaji wa masoko ya uhakika ya kuuzia biashara hizo”, alisema.

Katika kukabiliana na changamoto hizo, alisema Serikali itauimarisha Mfuko wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi kwa kuuongezea uwezo wa kutoa huduma zilizo bora kwa wananchi wengi zaidi.

“Kadhalika, tutawasajili wajasiriamali wote na kuwapatia vitambulisho. Pia, tutatoa mafunzo ya namna bora ya kuitumia mitaji na mikopo hiyo katika kupata vifaa na zana za kisasa na kuendesha shughuli za ujasiriamali kitaalamu zaidi, kulingana na mahitaji ya masoko ya wakati tulio nao”, alisema.

Aidha, alisema Serikali itawajengea wajasiriamali sehemu maalum za kufanyia biashara zao zitakazojengwa vizuri, ili waondokane na usumbufu wa kuhamahama huku na kule.

Sambamba na hilo, alisema kuwa pamoja na jitihada hizi, Serikali itawawekea mfumo na utaratibu bora wa kulipa kodi mara moja tu kwa mwaka na kuondosha ile kero ya utitiri wa kodi.

“Katika kuhakikisha kwamba mkakati huu unaleta ufanisi tunaoutarajia, tutakuwa tunafuatilia kwa karibu na kufanya tathmini ya mikopo tunayoitoa kwa vikundi hivyo, ili kujiridhisha endapo inawafikia walengwa na kwamba hakuna matumizi mabaya ya fedha hizo yanayofanywa na watumishi wa Serikali wasio waaminifu”, alisema.

Hata hivyo, aliitaka Idara inayohusika na mikopo isitosheke tu kutoa mikopo na mitaji na baadae kuripoti takwimu za vikundi vilivyopokea mikopo hiyo, na kuirejesha au kutoirejesha na badala yake aliitaka kujua mikopo hio imeleta faida gani kwa wananchi.

Huu ndio mfuko wa Uwezeshaji wananchi kiuchumi ambapo mwishoni mwa mwezi wa Disemba ulitimiza miaka saba tangu kuanzishwa kwake na kwenda sambamba na ile dhana ya Mapinduzi ya kuwawezesha wananchi kiuchumi sambamba na kujikwamua na umasikini uliokithiri.