SUZA: Chemchem ya kutoa wataalamu Zanzibar
Na Mohamed Mzee Ali, SUZA
Uoteshaji wa mti mkubwa wa matunda ulianza kwa fikra,ikapandwa mbegu, ukatoka mche ambao ulitunzwa kwa kutiliwa maji, mbolea na hatimae kuwa mti mkubwa unaotoa matunda kwa jamii.
Mnasaba kama huu ndivyo ilivyosadifu kwa Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar(SUZA),ambacho kimefikia miaka 21 tangu kuanzishwa kwake mwaka 2001 kwa sharia Namba 8, ambapo leo hii Zanzibar inafaidi matunda yake ikiwa ni utekelezaji wa dhamira ya Mapinduzi ya Januari 12, 1964 ya kuwapatia elimu ya juu watoto wa Zanzibar.
Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar(SUZA), kilianza kwa skuli moja tu ya Elimu lengo likiwa ni kukidhi haja ya walimu wenye viwango Zanzibar hasa katika masomo ya Sayansi na hisabati.
Skuli hiyo ilikuwa kama mche ambao ulitunzwa kwa kumwagiliwa maji na mbolea, na hivi sasa mti mkubwa umesimama ukiwa na matawi mengi na kusheheni matunda.
Tukiwa katika maadhimisho ya miaka 57 ya Mapinduzi, SUZA imepiga hatua kubwa ya kimaendeleo na kuwa chemchem ya kutoa wataalamu wa fani mbali mbali hapa Zanzibar.
Ikiwa imeanza na Skuli moja ya Elimu hivi sasa SUZA ina Skuli saba na Taasisi moja. Skuli hizo ni pamoja na Skuli ya Kilimo, Skuli ya Elimu,Taasisi ya Utalii, Skuli ya Kompyuta, Mawasiliano na Taaluma za Habari, Skuli ya Kiswahili na Lugha za Kigeni, Skuli ya Sayansi Asilia na Sayansi Jamii na Skuli ya Afya na Sayansi za Tiba.
Skuli hizo hivi sasa zina jumla ya Programu 56 katika ngazi mbali mbali ikiwemo Cheti, Stashahada, Shahada, Shahada ya Uzamili na pia SUZA inatoa Shahada ya Uzamivu(PhD).
Kutokana na program hizo Zanzibar imekuwa ikinufaika na wataalmu wake katika fani mbali mbali kupitia SUZA ikiwemo ya Afya na Tiba, Tehama, Kilimo, Elimu, Biashara , Sayansi na nyenginezo.
Mathalan katika mahafali ya 16 yaliyofanyika Disemba 30, 2020, jumla ya madaktari 48 wamehitimu mafunzo yao na kutunukiwa Shahada zao.
Madaktari hao wametanguliwa na idadi ya madaktari 25 wa awali waliosoma chuo hicho na kutunukiwa shahada zao katika mahafali zilizopita.
Aidha, SUZA imekuwa ikipata ongezeko la wanaojiunga na chuo hicho kila mwaka, ambapo wahitimu wa mwaka huu pekee ni 1524 kwa program zote 56 za chuo za Cheti, Stashahada, Shahada, Shahada ya Uzamili na Uzamivu .
Kabla ya kuanzishwa SUZA, Zanzibar ilikuwa ikitegemea zaidi vyuo vya Tanzania Bara na nje ya nchi katika fani mbali mbali. Vyuo hivyo ni kama Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Mzumbe, Ushirika Moshi, Sokoine na kadhalika.
Kwa upande wa nje ya Tanzania, wanafunzi wengi wa Zanzibar walikuwa wakisoma China, Sudan, Misri, Malaysia, Saud Arabia, UAE, Kuwait, Uingereza, Uganda na nchi nyengine.
Katika mahafali ya Disemba 30, 2020 ambayo mgeni rasmi alikuwa Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dk. Hussein Ali Mwinyi, jumla ya wahitimu 28 wametunukiwa Shahada za Uzamivu katika Skuli mbali mbali.
Skuli hizo ni pamoja na Skuli ya Elimu 19, Skuli ya Kiswahili 2, Skuli ya Sayansi Asili na Sayansi Jamii 7 na waliohitimu Shahada ya Kwanza kwa fani mbali mbali ni wanafunzi 453.
Bila shaka wataalamu kama hawa waliotoka SUZA ni hazina kubwa kwa Zanzibar katika uimarishaji wa rasilimali watu, na cha msingi zaidi ni namna gani vijana hawa watatumika.
SUZA KWA “CENTRE OF EXCELLENCE IN KISWAHILI”
Mbali na kutoa wataalamu , lakini SUZA pia ni kituo imara cha Lugha ya Kiswahili.Hivi sasa idadi ya wanafunzi wa Kiswahili inaongezeka tafauti na ilivyokuwa zamani. Mwaka huu idadi ya wanafunzi waliomaliza Shahada ya Kiswahili na Elimu imefikia 10.
Aidha, waliohitimu Shahada ya Uzamivu ya Elimu katika ufundishaji wa Kiswahili kwa wazungumzaji wa lugha nyengine mwaka huu ni wahitimu wanane, ambapo wanawake ni watano na wanaume watatu. Hatua hii inaonesha kwamba Kiswahili kimefahamika kuwa ni bidhaa muhimu ambayo Wazanzibari wanapaswa kuichangamkia katika soko la nje.
Sambamba na hilo, Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar(SUZA) kimo mbioni kutekeleza agizo la aliyekuwa Mkuu wa chuo hicho Dk. Ali Mohamed Shein wakati wa kuagwa hapo tarehe 6 Oktoba, 2020 la kuitaka SUZA ijidhatiti na kuwa “ Kituo kilichotukuka katika Lugha ya Kiswahili” yaani “Centre of Excellence in Kiswahili”.
Dk. Shein alisema kuwa anataka kuona Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar(SUZA) kinakuwa kama Chuo Kikuu cha Oxford, ambacho kimebobea katika lugha ya Kiingereza na makamusi yake kuaminika duniani kote.
Alisema Kiswahili nacho kichukue heshima kubwa kama hiyo kupitia SUZA kama ilivyo kwa chuo cha Oxford kwa Kiingereza, na kusisitiza tafiti zifanywe za kukuza zaidi lugha ya Kiswahili na kuchapisha machapisho kama ya Oxford.
Inawezekana hatua hiyo ikafikiwa, kwani tayari SUZA imeshatoa wahitumu wa Shahada ya Uzamivu katika Lugha ya Kiswahili, ambapo wengi wao ni wahadhiri wa chuo hicho na mwengine ni Katibu Mtendaji wa Baraza la Kiswahili Zanzibar.
SUZA NA USHIRIKIANO NA VYUO VYA NJE
Aidha , SUZA katika kujiimarisha na kukuza taaluma kimefanya ushirikiano na vyuo mbali mbali duniani. Vyuo hivyo ni pamoja na chuo cha Osman Gazi cha Uturuki, UDSM, UDOM, University of Rwanda , SUA, Upsala cha Finland na kadhalika.
SUZA pia imekuwa na ushirikiano wa karibu na taasisi na nchi mbali mbali duniani zote zikiwa na lengo la kuikuza na kuiendeleza taasisi hiyo ya elimu Zanzibar,ambayo ndio chimbuko la wataalamu. Bila shaka ushirikiano huu ni kwa kuzidi kupata mafanikio.
Miongoni mwa Taasisi zenye ushirikiano na SUZA ni pamoja na Benki ya Dunia(WB), Unicef, NORAD, DANIDA,Save the Children, Milele Foundation na COSTECH.
Aidha, SUZA imejenga ushirikiano na baadhi ya balozi za nje kama Ubalozi wa Denmark, Norway, Italia, Oman, China, India, Uturuki na Umoja wa Ulaya(EU).
SUZA KUJIANDAA KWA UCHUMI WA BULUU
SUZA katika mahafali yake 16 hapo Disemba 30, 2020, Mkuu wa chuo hicho aliyetawazwa hivi karibuni Mheshimiwa Dk. Hussein Ali Mwinyi, katika hotuba yake aligusia haja ya chuo hicho kusomesha elimu ya bahari na uvuvi ili vijana wa Zanzibar waingie katika uchumi wa buluu wakiwa weledi wa masuala hayo.
Alisema nchi kama Zanzibar haiwezekani ikawa haina wataalamu waliobobea katika fani za uvuvi na sayansi ya baharini, kwani Zanzibar ni kisiwa na sera iliyopo hivi sasa ni utekelzaji wa uchumi wa buluu.
Alifahamisha kuwa Zanzibar wakati huo iliibadilisha Skuli ya Lumumba kuwa chuo cha Uvuvi mnamo miaka ya mwishoni mwa 70s, lakini bahati mbaya elimu hiyo haikuendelezwa.
Hivyo, alisema kwa wakati huu Zanzibar ikiwa inatekeleza sera yake ya kuinua uchumi na maendeleo kupitia uchumi wa buluu, kuna haja kubwa ya kurudishwa elimu ya uvuvi na sayansi ya bahari kupitia SUZA.
CHANGAMOTO NA UTATUZI WAKE
SUZA kama zilivyo taasisi nyengine na penye mafanikio pia hapakosi changamoto, nayo katika uhai wake wa miaka 21 imekumbana na changamoto nyingi, lakini safari bado inaendelea.
Miongoni mwa changamoto inazokabiliana nazo SUZA ni pamoja na kutokuwa na dakhalia kwa baadhi ya kampasi zake , upungufu wa rasilimali fedha, ukosefu na ufinyu wa ofisi kwa wahadhiri wake na tafauti ya maslahi na vyuo vyengine vya serikali.
Pamoja na hayo wahadhiri wake wako imara na wamefumbia macho vishawishi vya kuhamia vyuo vyengine wakiwa ni waumini wa ‘uzalendo kwanza’.
Hata hivyo, changamoto zote hizi zinatatuliwa hatua kwa hatua kwa kushirikiana na serikali na taasisi binafsi hasa katika suala la majengo ya dakhalia za wanafunzi.
Matumaini ya Awamu ya Nane kwa SUZA ni makubwa kwa utatuzi wa changamoto hizo ili kuweka mazingira bora ya kujifunzia. Hii inatokana na kwamba mkuu wa Chuo pia ni mwanataaluma katika fani ya Udaktari wa binadamu kwa Shahada ya Uzamivu.
Aidha,pamoja na changamoto hizo, chuo kinasonga mbele kwa mafanikio makubwa, na kubaki kuwa chemchem ya kutoa wataalamu Zanzibar.