NA TATU MAKAME

MACHANO Juma Mtwana (25) mkaazi wa Donge Wilaya ya Kaskazini ‘B’ Unguja anashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoa wa Kaskazini Unguja kwa tuhuma za kupatikana na dawa za kulevya.

Akithibitisha tukio hilo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kaskazini Unguja, Kamishna Msaidizi wa Polisi, (ACP) Haji Abdalla Haji, alisema tukio hilo lilitokea Januari 24, mwaka huu majira ya saa 5:15 asubuhi huko Donge.

Alisema siku hiyo mtuhumiwa huyo alipatikana na kete 63 zinazosadikiwa kuwa ni dawa za kulevya jambo ambalo ni kinyume na sheria.

Alifahamisha kuwa kijana huyo alikamatwa kufuatia operesheni iliyofanywa na kitengo cha jeshi la polisi cha kupambana na wasambazaji, watumiaji na wauzaji wa dawa za kulevya katika mkoa huo.

Alibainisha kuwa siku hiyo kijana huyo alipatikana na dawa ambazo alizihifadhi ndani ya kifuko cha plastiki rangi nyeupe kisha kuweka kwenye kofia yake ya pama aliyokuwa ameivaa.

Hata hivyo Kamanda huyo alisema mtuhumiwa atafikishwa mahakamani taratibu zitakapokamilika na sasa yupo chini ya ulinzi wa jeshi la polisi.

Kamanda Haji aliwataka vijana kuacha kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya na watafute kazi nyengine za kufanya.

Nao wananchi wa mkoa huo walilitaka jeshi la Polisi kuwachukulia hatua kali watu wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya kwani wanaendelea kushajihisha matumizi ya dawa za kulevya.