NA KHAMISUU ABDALLAH

VIJANA nchini wamesisitizwa kutumia fursa zilizopo katika dhana ya uchumi wa buluu ili kujiajiri na kujikwamua na umasikini.

Ombi hilo limetolewa na Mwanzilishi wa taasisi ya Mimi na Mwinyi ambae pia ni Mkurugenzi Mkuu wa taasisi hiyo, Salmin Botea, wakati wanachama wa taasisi hiyo walipofanya ziara katika mabwawa ya ufugaji wa samaki na kasa Jozani, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 57 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Alisema, katika sekta ya bahari kuna fursa nyingi hivyo vijana wakiitumia vizuri, wataondokana na kadhia ya ukosefu wa ajira.

“Sasa ni wakati wetu vijana, tunachotakiwa ni kuamka na kutumia fursa hizi na sio wakati wa kukaa maskani,” alieleza Botea.

Alibainisha kwamba, sera ya serikali ya awamu ya nane inayoongozwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, ni kutumia fursa zilizomo katika dhana hiyo ili kukuza uchumi wa nchi na watu wake.

Alisema lengo la ziara hiyo ni kujifunza namna ya ufugaji bora wa samaki, kuwakuza na kuwalinda kasa ambao ni miongoni mwa viumbe ambayo dunia inawalinda.

“Kasa hivi sasa kutokana na binadamu kuwala kwa wingi viumbe hao na kufahamu namna bora ya uendeshaji wa miradi ya samaki.

Akizungumzia lengo la taasisi hiyo alisema ni kwenda sambamba na mitazamo ya serikali ya Dk. Mwinyi ambayo inahamasisha uanzishwaji wa miradi ya kiuchumi ikiwemo ya ufugaji wa samaki.

Hata hivyo aliwashauri viongozi wa majimbo kuanzisha miradi ambayo itawanufaisha vijana wa majimbo yao ili kutimiza lengo lililowekwa katika ilani ya uchaguzi ya CCM ya 2020/2025.

Naye Katibu Mstaafu wa Jumuiya ya Wenye Mashamba Jozani (UWEMAJO) na Muongozaji watalii Mohammed Haji, alisema uzalishaji samaki una faida kubwa kwa jamii na katika sekta nzima ya utalii.

Alisema aina nzuri ya samaki wa kufuga ni wale wanaohimili changamoto za mchanganyiko wa maji, akiwemo mkizi huku akibainisha kwamba samaki aina ya changu wakipata maji ya mvua wanakufa.

Akizungumzia changamoto zinazowakabili katika ufugaji wao alisema ni ukosefu wa vifaranga vya samaki na kuamini kwamba mwaka ujao Zanzibar itakuwa na vifaranga wengi wa samaki kutokana na kuongezeka kwa uzalishaji.

Alisema lengo lao ni kuwatunza kasa na baadae kuwarejesha baharini kwenye makaazi yao ya asili na kuipongeza taasisi ya ‘Mimi na Mwinyi’ kwa kuamua kujifunza namna ya kutumia rasilimali za bahari hasa ufugaji na kuwaomba kutovunjika moyo kuanzisha miradi ya ufugaji ambayo itawawezesha kujiajiri na kujipatia kipato.