NA HAFSA GOLO

SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar imesema itahakikisha utekelezaji wa awamu ya pili ya mradi wa TASAF utaangalia mahitaji ya walengwa wanaostahiki kupatiwa huduma zikiwemo za fedha taslimu.

Hatua hiyo imeelezwa itakwenda sambamba na ushirikishwaji wa wakaazi wa vijijini husika ili serikali wapatikane walengwa ndio wanaostahiki katika mradi huo.

Waziri  wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Sera, Utatibu na Baraza la Wawakilishi Dk. Khalid Salum Mohamed, alieleza hayo wakati akizungumza na wajumbe wa Kamati ya kusimamia ofisi za Viongozi Wakuu wa Serikali katika ukumbi wa ofisi hiyo Vuga, Zanzibar.

Alisema  utekelezaji huo unalenga kuimarisha maisha ya kaya maskini  kupitia  mradi huo yanatimia na watendaji wanaosimamia jukumu hilo  wanatimiza   masharti na vigezo vilivyowekwa katika kuzifikia kaya hizo .

Dk. Khalid alisema, eneo jengine ambalo litasimamiwa ipasavyo ni kuona  miradi yote  inayoekezwa ndani ya jamii iwe yenye mahitaji ya watu  katika maeneo husika na kuleta manufaa ndani ya jamii.

Alisema, katika mradi inayoekezwa na TASAF   hatokuwa tayari kuona inafata matakwa ya viongozi wa majimbo ama watendaji wa serikali kwa kuangalia maslahi binafsi badala yake itazingatia sheria na miongozo iliyowekwa na serikali.

“Lazima viongozi na watendaji wanaosimamia TASAF wafuate sheria na taratibu zilizopo bila ya kujali ama kuangalia maslahi binafsi ya viongozi,” alieleza waziri huyo.

Akizungumzia kuhusu fedha za mfuko wa jimbo, Dk. Khalid alisema ofisi yake haitokuwa na mzaha wala muhali badala yake itahakikisha inasimamia sheria na taratibu zilizowekwa.

“Nitakuwa mkali na kufuatilia kwa karibu matumizi ya fedha za mfuko wa jimbo kwani zinatolewa kwa ajili ya kuimarisha huduma za jamii hivyo viongozi lazima tuheshimu sheria zilizopo,” alisema.

Nae Mratibu wa TASAF Ofisi ya Makamu wa Pili, Khalid Hamrani alisema mradi wa awamu ya pili ya mrai huo, utawashirikisha ipasavyo  watendaji wa ofisi hiyo na ambae atabainika kwenda kinyume atachukuliwa hatua za kinidhamu na kisheria.

Alisema hatua hiyo imekuja baada ya kubaini kuwepo kwa changamoto zilizojitokeza katika mradi uliomalizika kwa kuorodheshwa watu wengine ambao waliokuwa sio walengwa.

“Waajiriwa wa serikali katika ofisi yetu ndio tutakaowatumia na asiewajibika vyema sheria itachukua mkondo wake ikiwa ni pamoja na kukatwa mshahara pale itapobainika ametoa fedha kwa mtu ambae sio mlengwa,” alisema.

Alifahamisha kuwa mradi huo ambao unatarajiwa kuanza kutekelezwa Febuari mwaka huu tayari uhakiki umeshafanywa na hata hivyo zoezi la kushirikishwa jamii katika utambuzi wa walengwa litasimamiwa ipasavyo.

Alifahamisha miongoni mwa mambo mengine yatakayotekelezwa katika mradi huo awamu hii ni kutumia teknolojia kuwatambua ili kuthibiti watu wasio walengwa.

Alisema utafiti uliofanywa umebaini Zanzibar kulikuwa hakuna wanufaika hewa ndani ya mradi huo isipokuwa kulikuwa na idadi kubwa ya walengwa wasiostahiki hali iliyochangiwa na wasimamizi wa walengwa wa mradi huo (SMC).

Alisema watu wengine waliobainika katika utafiti huo ni kuandikishwa watu wasio na sifa ya kuingia katika mradi huo.

Mapema Mwakilishi wa jimbo la Ziwani, Suleiman Makame Ali, alimuomba Dk. Khalid kusimamia kwa karibu mradi huo hasa ikizingatiwa wapo baadhi ya masheha wamekuwa wakitumia fursa hiyo kwa kuingiza familia au watu wakatibu na wale walengwa wakaendelea kukosa kuitumia fursa hiyo.