NA MWANAJUMA MMANGA

MSICHANA (15) mkaazi wa Kibele anadaiwa kuambukizwa virusi vya UKIMWI baada ya kutoroshwa, kubakwa na kulawitiwa na kijana aliyetambulika kwa jina Boniface Simon Sheba (16) mkaazi wa Bungi.

Akizungumza na waandishi wa habari mkuu wa dawati la Jinsia la polisi mkoa wa Kusini Unguja, Ali Mohammed Othman, alisema msichana huyo baada ya kubakwa na kulawitiwa alichukuliwa na kupelekwa katika hospitali ya Mnazimmoja kwa ajili ya uchunguzi.

Aidha alisema baada ya kuchunguzwa msichana huyo ilithibitika kuwa amebakwa na kuwa ameathirika kwa kuambukizwa virusi vya UKIMWI.

Alisema mkuu huyo kuwa msichana huyo alitoroshwa akiwa chini ya ulinzi wa wazazi wake na kukimbia kwenda kulala kwa mwanamme wake huko maeneo ya Bungi.

Alisema binti huyo alitoroshwa na inavyosemekana ametoroshwa mara mbili ambapo mara ya mwanzo alitoroshwa katika mkesha wa mwaka mpya mwaka huu.

 “Binti huyo alitoroshwa tena kwa mara ya pili siku za hivi karibuni na mwanamme huyo huyo na mara baada  ya kumtafuta  wazazi wake ndipo walipoelekezwa binti huyo ameonekana maeneo ya Bungi” alisema Mkuu wa dawati huyo.

Alifahamisha kuwa walikwenda Bungi kwa bahati mbaya asubuhi walipokwenda hawakumuona kutokana na mtoto huyo ameshaondoka kwenda kwa shangazi yake na baadae wakakusanyana familia yake na kwenda dawati la polisi huko Tunguu.

Alisema dawati hilo likachukua hatua za awali za kuchukua maelezo yao na kumpeleka hospitali ya Mnazimmoja kwa ajili ya kuangaliwa vipimo vya damu na masuala ya kuingiliwa na kuonekana ana virusi vya UKIMWI.

Aidha alisema baada ya kubainika binti huyo muathirika ndipo walipomchukua mwanamme naye kwenda kuchunguzwa afya na kupata taarifa za awali bado yuko salama.

Alisema ya kesi ya binti hiyo imefunguliwa Januari 11 mwaka huu katika kituo cha polisi Unguja Ukuu lakini kwa mara kwanza watuhumiwa walikwenda kituo cha polisi Tunguu.

Mkuu huyo alisema kutokana na jalada kwa utaratibu wao zoni ya tukio hilo limetokea Tunguu lakini shauri wamelihamishia Unguja Ukuu.

Alisema watoto wa siku hizi wana changamoto zao lakini kwa taarifa za wazazi wake siku ya mkesha wa mwaka mpya alitoroka tu bila ya kuaga na kuelekea kwa mvulana huyo.