MOSCOW, URUSI

MKOSOAJI wa Serikali ya Urusi Alexei Navalny amewahimiza Warusi kuingia barabarani katika maandamano baada ya jaji kumuweka rumande kwa siku 30 kabla ya kesi yake kuanza licha ya miito kutoka kwa nchi za magharibi ya kutaka mwanasiasa huyo wa upinzani aachiliwe huru.

Umoja wa Mataifa na nchi za Magharibi ziliiambia Urusi kabla ya uamuzi huo wa mahakama imuwachilie huru Navalny, na baadhi ya nchi zilitoa wito wa kutangazwa vikwazo vipya dhidi ya Urusi, ambayo iliwaambia wayafikirie mambo yanayowahusu wao.

Uamuzi wa kumuweka rumande kwa kukiuka masharti ya hukumu ya adhabu iliyoahirishwa ya kufungwa jela, siku moja baada ya kurejea Urusi kwa mara ya kwanza kufuatia tukio la kupewa sumu inayoathiri mishipa ya fahamu mwaka jana, huenda ukawa utangulizi wa kumfunga jela kwa miaka mingi.