NA MWAJUMA JUMA

TIMU ya soka ya Mlandege imewatambia maafande wa Polisi kwa kuwafunga bao 1-0.

Mchezo huo ambao ni wa ligi kuu ya Zanzibar ulichezwa katika uwanja wa Mao Zedong A ambao ulikuwa wa  ushindani.

Miamba hiyo ilikianza kipindi cha kwanza kwa kushambuliana kwa zamu kila mmoja akisaka bao la ushindi na kuufanya mchezo kuwa mgumu.

Katika mchezo huo Mlandege bao lake liliwekwa kimiyani na Abdulmajid Juma Haji dakika ya 41.

Ushindi huo Mlandege umewafanya wavuke hatua moja juu kwa kuwa nafasi ya 11 pointi nane.

Huo ni ushindi wa pili kwa Mlandege ambayo imecheza mechi tisa licha ya kuwa na mchezo mmoja mkononi, ambapo kati ya michezo hiyo imefungwa mitano na sare mbili.

Mbali na mchezo huo pia katika uwanja wa Amaan kulikuwa na mchezo kati ya Malindi na Zimamoto ambao ulimalizika kwa sare ya kutokufungana.

Kwa matokeo hayo Zimamoto imefikisha pointi 13 na kupanda hadi nafasi ya saba kutoka ya nane wakati Malindi imefikisha pointi 14 na kuendelea kubakia katika nafasi ya sita ya msimamo wa ligi hiyo inayoongozwa na KMKM wenye pointi 19.

Ligi hiyo itaendelea tena leo kwa kupigwa michezo  miwili, ambapo dimba la Amaan saa 10 :00 Alasiri Kipanga itacheza na Black Sailor, na uwanja wa Mao Zedong  saa 10:00 Alasiri KVZ itawaalika Mafunzo.