NA KHAMISUU ABDALLAH

MAWAZIRI wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar wameshauriwa kuziangalia sheria ambazo kandamizi na hazitekelezeki ili zifanyiwe marekebisho zilete tija kwa maslahi ya nchi na watu wake.

Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar, Catherine Peter Nao, alitoa ombi hilo wakati akizungumza na Zanzibar leo ofisini kwake Kisiwandui mjini Unguja.

Alisema imefika wakati kwa kila waziri kukaa na wanasheria wa wizara zao kuzipitia sheria zao ili baraza linalokuja waziwasilishe na kufanyiwa marekebisho.

Aidha alisema kuna sheria i ambazo hazina maslahi kwa wananchi hali ambayo inapelekea watu kukosa haki zao.

“Sheria zote ambazo hazina maslahi ni wakati kwa mawaziri kuzifanyia kazi na kuzipeleka katika chombo cha kutunga sheria ili kufumuliwa na kuwekwa sawa ili ziweze kufanya kazi vizuri,” alisema. 

Alibainisha kuwa ni aibu kwa Zanzibar hadi leo unaposikiliza vyombo vya habari jambo la udhalilishaji limekuwa ni kitu cha kawaida na kuwa kama nyimbo hali ambayo inatokana na sheria kutofanya kazi vizuri.

Alisema sheria zilizotungwa hasa ya udhalilishaji zina kasoro kwani imeeleza wazi mtuhumiwa wa kitendo hicho habaswi kupatiwa dhamana na atakapotiwa hatiani miaka 30 jela lakini sheria hiyo hiyo inamtoa kwa kumpa dhamana.

Catherine alibainisha kuwa kumpa dhamana mbakaji wa udhalilishaji ni kumbembeleza na kumpa mwanya wa kuendelea kuwadhalilisha na wengine.

“Kuna sheria ambayo inaeleza ukitaka kuteuliwa Mkuu wa Mkoa au wilaya ni lazima uwe umehudumu miaka saba mpaka tisa ile sio sheria mimi sikusoma lakini ikiletwa naipinga moja kwa moja waliotunga hawakuwa makini walisahau kama tuna watoto ambao wamesoma na wanaelimu kubwa,” alisema.

Aliongeza kuwa; “Zipo sheria nyingi hazitekelezi mpaka zimesababisha serikali inafikishwa mahakamani kutokana na sheria mbovu, sasa wakati umefika kuzifanyia marekebisho kwa maslahi ya nchi yetu na sio kwa maslahi ya mtu,” alisisitiza

Hivyo, aliwaomba wajumbe wa baraza la Wawakilishi wapya kushirikiana na wawakilishi wa zamani ili kuona mapungufu ya sheria hiyo yanafanyiwa kazi mara moja.

“Kila kwenye sheria haipo sawa ni wakati kuona wazitafuta na kuzifanyia marekebiaho washirikiane pamoja kuona mapungufu haya yanaondoka” alisisitiza.

Sambamba na hayo aliwasisitiza wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kupitisha sheria kwa maslahi ya vizazi ya sasa na baadae na sio kutunga sheria kwa maslahi yao binafsi.

Akizungumzia ushauri huo, Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Mgeni Hassan Juma, alisema serikali ina uwezo wa kupeleka sheria na kuzipitisha na hata wajumbe kuwa na uwezo wa kupeleka hoja binafsi ili kuitaka serikali kufanya mabadiliko ya sheria hizo.

Aidha alisema Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi mara nyingi amekuwa akizungumza suala la sheria na kuonekana nyingi zina mapungufu hasa sheria ya udhalilishaji.

Alitumia muda huo kuiomba serikali na tasisi zinazoshughulikia masuala ya udhalilishaji kushirikiana na Baraza la Wawakilishi katika kuifanyia marehekebisho sheria kwani imeonekana bado haikidhi haja na kusimamia vizuri ili kuona vitendo vya udhalilishaji Zanzibar vinaondoka.