NA MWAJUMA JUMA

KOCHA Mkuu wa timu ya soka ya Namungo Hemed Suleiman Moroko amesema kutokuwa makini kwa wachezaji wake kwenye umaliziaji ndio iliyopelekea timu yake kupoteza mchezo dhidi ya Simba.

Namungo ilicheza mchezo wa nusu fainali ya michuano ya kombe la mapinduzi na Simba na kuruhusu kufungwa, mabao 2-1, katika mchezo huo ambao ulichezwa kwenye uwanja wa Amaan.

Moroko alisema katika mchezo huo wachezaji wake walicheza vizuri na kujituma na makosa yaliojitokeza ni matokeo ya mchezo huo.

“Nilijuwa kama Simba itakuja na presha kubwa tulijaribu kuwazuwia lakini hatukuweza kuingia kwenye mchezo mapema na tulifanya makosa lakini ndio mchezo”, alisema.

Aidha alisema mashindano hayo yamewasaidia sana kujenga timu lakini wachezaji wake kutokuwa makini kwenye umaliziaji kumewafanya kushindwa kufika fainali.

Alisema kipindi cha kwanza waliruhusu kufungwa na walipoingia kipindi cha pili walijaribu sana kushambulia lakini walikosa nafasi.

Namungo ambayo ni mara yake ya kwanza kushiriki michuano ya mapinduzi ilitinga hatua ya nusu fainali baada ya kupata na nafasi ya mshindwa bora (Best Looser), ambapo katika mchezo huo ilifungwa mabao 2-1.